Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na wajinga hawa wanasema yule mwenye kupinga kufufuliwa anakufuru na kuuawa, hata kama atasema “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah”, na yule mwenye kupinga chochote katika nguzo za Uislamu amekufuru na kuuawa, hata ikiwa ataitamka [Shahaadah]. Vipi basi isimfae ikiwa kapinga kitu katika mambo ya matawi, lakini imfae akipinga Tawhiyd ambayo ndio msingi na asili ya dini ya Mitume?

MAELEZO

Hapa hawa watu wajinga wametumbukia katika mkanganyiko na dalili yao inatumiwa dhidi yao wenyewe. Wanasema kuwa mwenye kupinga kufufuliwa anauawa kafiri. Wanasema kadhalika juu ya yule mwenye kukanusha kitu katika nguzo za Uislamu hata kama atasema kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah. Vipi basi asikufurishwe wala kuuawa yule mwenye kukanusha Tawhiyd ambayo ndio msingi wa dini, hata kama mtu atasema hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah? Je, mtu huyu si mwenye kustahiki zaidi kuwa kafiri kuliko yule mwenye kupinga uwajibu wa swalah na zakaah? Haya ni malazimisho ambayo hawawezi kuyaepuka.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 93
  • Imechapishwa: 28/11/2023