Miongoni mwa mambo yanayofahamisha fadhilah za masiku haya kumi kutoka katika Hadiyth hizi ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuwa alikuwa akiwaamsha familia yake kwa ajili ya kuswali na kufnaya Dhikr kwa ajili ya kupupia kutumia fursa ya nyusiku hizi zilizobarikiwa kwa ´ibaadah zinazostahiki. Kwani ni fursa ya umri na ngawira kwa yule ambaye amewafikishwa na Allaah (´Azza wa Jall).

Kwa hivyo haitakiwi kwa muumini mwenye akili kujikosesha yeye na familia yake fursa hii adhimu, kwa si vyengine isipokuwa ni nyusiku chache tu. Pengine mtu akapata zawadi miongoni mwa zawadi za Allaah na hivyo ikawa ndio sababu ya kufaulu kwake duniani na Aakhirah.

Hakika ni katika kunyimwa kukubwa na khasara kubwa kuona waislamu wengi wanatumia wakati huu wenye thamani katika mambo yasiyowanufaisha. Wanakesha sehemu kubwa ya usiku katika burudani za batili. Unapofika wakati wa kusimama kuswali usiku wanalala na wanajikosesha kheri nyingi. Huenda wasiyapate kabisa masiku haya katika mwaka wao huu. Hivi ndivo shaytwaan anavowafanyia vitimbi, kuwazuilia kutokamana na njia ya Allaah na kuwapotosha. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ إِلَّا مَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْغَاوِينَ

”Hakika Waja Wangu huna mamlaka nao isipokuwa ambaye atakufuata katika waliopotoka.”[1]

Mwenye busara haimfanyi shaytwaan kuwa ni kipenzi badala ya Allaah pamoja na kwamba anajua kuwa yeye ni adui yake. Kufanya hivo kunapingana na akili na imani. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا

”Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake kuwa walinzi wapenzi badala Yangu na hali wao kwenu ni maadui? – Ni ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu!”[2]

إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ

“Hakika shaytwaan kwenu ni adui, hivyo basi [nyinyi] mfanyeni kuwa ni adui. Hakika anaitia kikosi chake [wanaomtii] ili wawe watu wa Motouwakao kwa nguvu.”[3]

[1] 15:42

[2] 18:50

[3] 35:06

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 155
  • Imechapishwa: 09/03/2024