Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ataombea Ummah wake kwa wale walioingia Motoni katika watu wenye madhambi makubwa. Watatolewa kwa uombezi wake baada ya kuchomwa na kuwa mkaa na majivu, kisha wataingia Peponi kwa uombezi wake. Mitume wengine, waumini na Malaika watakuwa na uombezi pia. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“Na wala hawamuombei uombezi yeyote yule isipokuwa yule Anayemridhia.”[1]

Kafiri hautomfaa kitu uombezi wa wenye kuombea.

MAELEZO

Uombezi maana yake kilugha ni kuifanya witr shufwa. Uombezi maana yake kiistilahi ni kukaa katikati kwa ajili ya mwingine kwa ajili ya kuleta manufaa na kuzuia madhara. Kuna aina mbili za uombezi wa siku ya Qiyaamah:

1 – Uombezi ambao ni maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

2 – Uombezi wenye kuenea kwake na kwa wengine.

Uombezi ambao ni maalum kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni uombezi wake mkubwa kwa Allaah juu ya wale waliosimama katika uwanja ili ahukumu kati yao. Hapo ni pale ambapo watapatwa na dhiki na uzito ambao hawatouweza. Matokeo yake wataenda kwa Aadam, Nuuh, Ibraahiym, Muusa na ´Iysaa ambapo wote watake udhuru. Baada yao wataenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye atawaombea kwa Allaah. Kisha aje (Subhaanah) kuhukumu kati ya waja Wake.

Sifa hiyo imetajwa katika Hadiyth ya parapanda inayotambulika. Lakini cheni ya wapokezi wake ni dhaifu imetiwa dosari[2] na imeondoshwa katika Hadiyth Swahiyh na ikafupishwa kutaja uombezi kwa wale watenda madhambi makubwa. Ibn Kathiyr na mfafanuzi wa “at-Twahaawiyyah” wamesema:

“Malengo ya Salaf kukomeka kutaja uombezi kwa watenda madhambi makubwa ilikuwa kuwaraddi Khawaarij na wale wanaowafuata katika Mu´tazilah.”

Uombezi huu haukanushwi na Mu´tazilah na Khawaarij na kumeshurutishwa juu yake idhini ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”[3]

[1] 21:28

[2] Ni Hadiyth ndefu sana na katika cheni ya wapokezi wake yuko Ismaa´iyl bin Raafiy´, ambaye ni dhaifu, na Muhammad bin Yaziyd au Ziyaad, ambaye hajulikani. Ibn Kathiyr ameitaja katika ”Tafsiyr” yake (02/146-148) kutoka kwa at-Twabaraaniy na akasema:

”Hadiyth hii inatambulika lakini ni geni sana. Baadhi ya sehemu zake zina yenye kuyatilia nguvu katika Hadiyth mbalimbali. Katika baadhi ya matamshi yake kuna udhaifu.”

Rejea ”an-Nihaayah” (01/253) ya Ibn Kathiyr.

[3] 02:255

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 128-129
  • Imechapishwa: 04/12/2022