Swali 81: Baadhi ya watu wanaelewa maana ya maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَلَا يَخَافُونَ لَوْمَةَ لَائِمٍ

”… na wala hawakhofu lawama ya mwenye kulaumu.”[1]

ya kwamba inahusiana na wale wanaotaja makosa ya watawala juu ya mimbari na mbele ya umati wa watu. Wanafupisha jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu katika suala hilo. Tunataraji kuwanasihi vijana hao na kuwawekea wazi maana sahihi ya Aayah hii. Na ni ipi hukumu ya wale wanaowazungumza watawala hadharani?

Jibu: Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَن يَرْتَدَّ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّـهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَافِرِينَ يُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا يَخَافُونَ لَوْمَةَ لَائِمٍ

”Enyi mlioamini! Yeyote atakayeritadi miongoni mwenu kutoka dini yake, basi Allaah atawaleta watu [badala yao] Atakaowapenda nao watampenda; wanyenyekevu kwa waumini, wenye nguvu juu ya makafiri; wanafanya jihaad katika njia ya Allaah na wala hawakhofu lawama ya mwenye kulaumu.”

Aayah hii inamuhusu kila ambaye anawapiga vita wenye kuritadi, akaongea neno la haki, akapambana katika njia ya Allaah, akaamrisha mema na kukemea maovu kwa ajili ya kumtii Allaah, asiache kutoa nasaha, kuamrisha mema, kukataza maovu na kupambana jihaad katika njia ya Allaah kwa ajili ya watu au kwa ajili ya kuwaogopa watu. Lakini jambo la kutoa nasaha na kulingania kwa Allaah ni lazima liafikiane na maneno Yake (Ta´ala):

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[2]

Allaah (Subhaanahu  wa Ta´ala) alisema kumwambia Muusa na Haaruun (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) alipowatuma kwa Fir´awn:

فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ

“Mwambieni maneno laini huenda akawaidhika au akaogopa.”[3]

Amesema (Ta´ala) kumwambia Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ

”Basi ni kwa rehema kutoka kwa Allaah umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelikukimbia.”[4]

Nasaha kwa watawala zinatakiwa ziwe kwa siri. Haitakiwi kuwafedhehesha. Haitakiwi kwa wajinga na watu wasiokuwa na elimu kuhamasika dhidi yao. Nasaha zinatakiwa ziwe kwa siri kati ya mwenye kutoa nasaha na mtawala, ima kwa mdomo au kwa kuwaandikia. Aidha hilo linatakiwa kufanyika kwa urafiki na adabu. Ama kuwasema vibaya watawala juu ya mimbari na katika mihadhara yenye kuenea sio nasaha bali ni kukashifu. Mambo kama hayo ni fitina na chuki kati ya watawala na wananchi na linapelekea katika madhara makubwa. Huenda hilo likapelekea watawala kuwavamia wanazuoni na walinganizi. Mambo kama hayo yana madhara makubwa kuliko manufaa.

Endapo utamzungumzia mtenda dhambi wa kawaida mbele ya umati wa watu, basi kitendo chako hicho kitazingatiwa ni fedheha na sio nasaha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule mwenye kumsitiri muislamu, basi Allaah atamsitiri duniani na Aakhirah.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapotaka kuzindua jambo basi hamlengi mtu bali husema:

“Inakuweje wakawepo watu… ”[6]

Kwa sababu kuwataja watu kwa majina kunaharibu zaidi kuliko kunavotengeneza. Bali pengine kitendo hicho kisitengeneze kabisa. Bali ina madhara makubwa kwa mtu mmojammoja na jamii nzima.

Njia za nasaha zinatambulika. Wanasihiji ni lazima wawe na elimu, utambuzi na uelewa, kulinganisha kati ya manufaa na madhara, ni lazima watazame matukio yake. Pengine kitendo cha chenyewe cha kukemea maovu kikawa ni maovu, kama alivosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)[7]. Hapo ni pale ambapo maovu yatakemewa kwa njia isiyokubalika katika Shari´ah, basi kitendo chenyewe cha ukemeaji kinakuwa ni maovu kutokana na yale madhara yanayopelekea. Isitoshe nasaha kwa njia isiyokubalika katika Shari´ah tunaweza kuiita fedheha, uchochezi na kuongeza fitina.

[1] 5:54

[2] 16:125

[3] 20:44

[4] 3:159

[5] Muslim (2699).

[6] al-Bukhaariy (5063) na Muslim (1401).

[7] Ibn Taymiyyah amesema:

”Imesemekana kuwa kuamrisha kwako mema inatakiwa iwe mema na kukataza kwako maovu kusiwe maovu.” (al-Amr bil-Ma´ruuf wan-Nahiy ´an-il-Munkar, uk. 7)

Sufyaan ath-Thawriy amesema:

”Hakuna anayeamrisha mema na kukataza maovu isipokuwa anatakiwa awe na sifa tatu: kufanya urafiki wakati wa kuamrisha na kukataza, mwadilifu wakati wa kuamrisha na kukataza na mjuzi wakati wa kuamrisha na kukataza.” (al-Amr bil-Ma´ruuf wan-Nahiy ´an-il-Munkar, uk. 19)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 206-209
  • Imechapishwa: 22/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy