81. Mtazamo wa Jahmiyyah juu ya kuwepo kwa Pepo na Moto hivi sasa

´Aqiydah hii imekadhibishwa na Jahmiyyah wakanushaji ambao wamedai kuwa Pepo na Moto havijaumbwa hivi sasa. Wamesema kuwa vitaumbwa utapofika wakati vitapohitajika. Jahmiyyah na vifaranga vyao hawaamini eti kuumbwa kwa Pepo na Moto kabla ya wakazi wake kuingia ndani yake ni mchezo. Kwa msemo mwingine wamejengea nadharia yao kwa kutumia akili zao, wakayatupilia mbali Maandiko ya Qur-aan na Sunnah na wakapinga kuumbwa kwa Pepo na Moto hivi sasa. Kwa sababu wao wanaona kuwa haiwezekani kwa Allaah akaumba Pepo na Moto kisha baadaye akaviacha vitupu, kwa sababu wanaona kuwa kufanya hivo ni mchezo. Watu hawa hawakumuadhimisha Allaah vile anavyopasa kuadhimishwa. Allaah haumbi chochote wala hacheleweshi chochote isipokuwa kwa hekima – kwa sababu Yeye ndiye Mshindi, Mwenye hekima. Kwa hivyo huu ni msingi wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, nao ni kuamini kuwepo kwa Pepo na Moto na kwamba vimeshaumbwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pepo na Moto vilizozana ambapo Moto ukasema: “Ndani yangu wanaingia wakandamizaji na wenye kiburi.” Pepo nayo ikasema: “Ndani yangu wanaingia watu wadhaifu na wale masikini.” Ndipo Allaah (´Azza wa Jall) akasema: “Wewe ni adhabu Yangu ambayo namsibu yule Ninayemtaka.” Akasema kuiambia Pepo: “Wewe ni huruma Yangu ambayo namsibu yule Ninayemtaka. Kila mmoja wenu atajazwa.” Itapofika siku ya Qiyaamah basi Allaah (´Azza wa Jall) hatomdhulumu yeyote katika waja Wake kitu chochote. Kutatupwa Motoni na useme:

هَلْ مِن مَّزِيدٍ

“Hakuna zaidi?”

mpaka Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) aweke unyayo Wake. Hapo ndipo utajaa, ukusanyike na useme: “Tosha, tosha.”[1]

Hii ni dalili juu ya kuwepo kwa Pepo na Moto hivi sasa na kwamba vimeshaumbwa.

[1] ad-Daaraqutwniy katika ”Kitaab-us-Swifaat” (4).

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 174
  • Imechapishwa: 29/06/2026