Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Lakini kisa hiki kinatoa faida ya kwamba muislamu wa kawaida, bali hata mwanachuoni, anaweza kutumbukia katika aina ya shirki bila ya kujua. Vilevile kinatoa faida kujifunza na kuwa makini na kujua ya kwamba maneno ya mjinga “Tunajua Tawhiyd” ni katika ujinga mkubwa na hila za shaytwaan. Kinatoa faida pia ya kwamba muislamu akitamka kwa neno la kufuru na yeye hajui, akajua hilo na kutubia papo hapo ya kwamba hakufuru, kama walivyofanya wana wa israaiyl na wale waliomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kadhalika kinatoa faida pia ya kwamba lau ikiwa hakukufuru, akemewe [aliyesema maneno hayo] kwa makemeo makali kabisa, kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Yaliyopitika katika tukio la Dhaat Anwaatw na yaliyowafika wana wa israaiyl yanatoa faida mambo yafuatayo:

1 – Mtu, ni mamoja mwanachuoni na asiyekuwa mwanachuoni, anaweza kuwa mjinga wa baadhi ya aina za shirki. Hili linawajibisha kwa mtu kujifunza na kujua ili asije akatumbukia katika shirki pasi na kujua hilo. Kadhalika ni katika mambo ya khatari kabisa kwa mtu kusema kuwa anajua shirki ni kitu gani pamoja na kuwa sivyo hivyo, kwa sababu huu ni ujinga uliopandiana. Ujinga uliopandiana ni khatari zaidi kuliko ujinga mwepesi. Mtu aliye na ujinga mwepesi hujifunza na akawanufaisha wengine na elimu yake. Lakini mtu aliye na ujinga uliopandiana hujiona kuwa ni mjuzi, ilihali  ukweli wa mambo ni mjinga, hivyo matokeo yake akaendelea katika yale aliyomo katika matendo yanayopingana na Shari´ah.

2 – Muislamu akitamka tamko la kufuru na baada ya hapo akakumbushwa na akatubia papohapo, hadhuriki na hilo kwa sababu ya ujinga wake. Allaah haikalifishi nafsi zaidi ya vile inavyoweza. Ama akiendelea na kitendo chake cha kufuru, atahukumiwa kutokana vile hali yake inavyopelekea.

3 – Hata kama mtu hajui kuwa kile anachotaka kufikia ni kufuru, anatakiwa kukumbushwa kwa ukali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaambia Maswahabah zake:

“Allaah ni Mkubwa! Ni nyayo zilezile. Kwa hakika mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua.”

Haya ni makemeo ya wazi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 90-91
  • Imechapishwa: 28/11/2023