80. Ahl-us-Sunnah wanalingania katika maadili matukufu

Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Pamoja na misingi hii wanaamrisha mema na wanakataza maovu kwa yale ambayo Shari´ah imeyawajibisha.

Wanaonelea kufanya hijjah, kupigana jihaad, swalah ya ijumaa na sikukuu pamoja na viongozi, ni mamoja wakiwa wema au waovu. Wanahifadhi swalah za mkusanyiko na wanautakia ummah kheri.

MAELEZO

Maneno haya ambayo ameyataja mtunzi kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni maneno mazito. Ni maneno ambayo yanapaswa kuandikwa kwa maji ya dhahabu. Inampasa kwa kila muumini ayaamini, ayatendee kazi na ayafuate. Haya ndio maneno ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na yamefahamsihwa na Qur-aan na Sunnah. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye kusifika na kheri zote. Wanaamrisha mema na kukataza maovu kwa mujibu wa Shari´ah. Wamefungamana na Shari´ah. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanasimamisha swalah na wanatoa zakaah na wanamtii Allaah na Mtume Wake – hao Allaah atawarehemu. Kwani hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa aliyeshinda, Mwenye hekima.” (09:71)

Wanaonelea kufaa kusimamisha swalah ya ijumaa, swalah za mkusanyiko, kupigana jihaad pamoja na viongozi, ni mamoja wawe wema au waovu. Hayo yanapelekea katika kupambana jihaad, kuwepo kwa amani na umoja. Mzigo wa madhambi yake yanamuhusu yeye. Wanaswali pamoja naye swalah ya ijumaa na swalah za mkusanyiko hata kama atakuwa ni mwenye kufanya baadhi ya maasi. Hivi ndivyo hali ilivyokuwa wakati wa Banuu Umayyah na Banuul-´Abbaas.

Wanaamrisha kuwatendea wema wazazi wawili, kuunga kizazi, kufanya ujirani mwema, walingania katika kuwa na maadili mema, kufanya matendo mazuri, wanahimiza kumuunga yule aliyekukata, umsamehe yule aliyekudhulumu na umpe aliyekunyima.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 123-125
  • Imechapishwa: 03/11/2024