[10] Wakati wa swalah ya usiku unaanza baada ya swalah ya ´Ishaa mpaka swalah ya al-Fajr. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah amekuzidishieni swalah nayo ni Witr[1]. Iswalini kati ya swalah ya ´Ishaa na swalah ya Fajr.”[2]

[11] Lililo bora ni kuswali sehemu ya mwisho ya usiku kwa yule atayeweza kufanya hivo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anayechelea kutoweza kuamka sehemu ya mwisho ya usiku, basi aswali Witr mwanzo wake. Yule anayetumai kuamka mwisho wake, basi aswali sehemu ya mwisho ya usiku, kwa kuwa kuswali sehemu ya mwisho ya usiku kunashuhudiwa na ndio bora.”[3]

[12] Endapo mtu atakhiyarishwa kati ya kuswali na mkusanyiko mwanzoni mwa usiku na kuswali peke yake mwishoni mwa usiku, inahesabika kuswali na mkusanyiko ndio bora zaidi. Hili ni kwa sababu atalipwa kuwa ameswali usiku mzima, kama ilivyotangulia kwenye nambari nne kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kadhalika matendo ya Maswahabah yalikuwa juu ya hilo kama ilivyokuwa wakati wa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh). ´Abdur-Rahmaan bin ´Abd al-Qaariy amesema:

“Usiku mmoja nilitoka mimi pamoja na ´Umar bin al-Khattwaab kwenda msikitini na tukakuta watu wametawanyika; mwanamume anaswali peke yake na mwengine anaswali na mkusanyiko. Akasema: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba mimi naonelea kuwa lau mtu atawakusanya wote nyuma ya msomaji mmoja basi ingelikuwa bora.” Halafu akalishikilia na akawakusanya nyuma ya Ubayy bin Ka´b. Kisha usiku mwengine nikatoka naye na tukakuta watu wanaswali nyuma ya msomaji wao. Ndipo ´Umar akasema: “Ni uzuri wa uzushi uliyoje huu. Ile [sehemu ya usiku] wanayolala ni bora kuliko ile [sehemu] wanayoswali ndani yake.” – anamaanisha sehemu ya mwisho ya usiku, watu walikuwa wanaswali sehemu ya mwanzo wa usiku.”[4]

Zayd bin Wahb amesema:

“´Abdullaah alikuwa akituswalisha Ramadhaan na akimaliza inapokuwa usiku.”[5]

[1] Swalah ya usiku yote inaitwa “Witr” kwa kuwa idadi yake ni witiri.

[2] Hadiyth ni Swahiyh. Ameipokea Ahmad na wengineo kutoka kwa Abu Baswiyr. Imetajwa katika “as-Swahiyhah” (108) na “al-Irwaa´” (2/158).

[3] Muslim na wengineo. Imetajwa katika “as-Swahiyhah” (2610).

[4] al-Bukhaariy na wengineo. Imetajwa katika “at-Taraawiyh”, uk. 48.

[5] ´Abdur-Razzaaq (7741) na wengineo na mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh. Imaam Ahmad ameashiria upokezi huu na ulio kabla yake pindi alipoulizwa: “Je, mtu acheleweshe swalah mpaka sehemu ile ya mwisho ya usiku?” Akajibu: “Hapana. Mwenendo wa waislamu ni wenye kupendeza zaidi kwangu.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 25
  • Imechapishwa: 07/05/2019