[9] Ama kuhusu kisomo katika swalah ya usiku Ramadhaan na miezi mingine, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuweka kiwango maalum kwa njia ya kwamba mtu hatakiwi kuzidisha juu yake wala kupunguza. Kisomo chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na urefu wake ulikuwa unatofautiana. Wakati fulani alikuwa akisoma katika kila Rak´ah “al-Muzzammil” na Suurah hii ina Aayah ishirini na wakati mwingine akisoma kiasi cha Aayah khamsini. Alikuwa akisema:

“Atakayeswali usiku kwa Aayah mia moja basi hatoandikwa katika waghafilikaji.”

Katika Hadiyth nyingine:

“… kwa Aayah mia mbili ataandikiwa katika wema na wenye IKhlaasw.

Usiku mmoja pindi alipokuwa mgonjwa, alisoma (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zile Suurah saba, nazo ni “al-Baqarah”, “Aal ´Imraan”, “an-Nisaa´”, “al-Maaidah”, al-An´aam”, “al-A´raaf” na “at-Tawbah”.

Katika kisa cha Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ´anh) swalah yake nyuma ya Mtume (´alayhis-Swalaatu was-Salaam), alisoma (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Rak´ah moja “al-Baqarah”, “an-Nisaa´” na “Aal ´Imraan” taratibu[1].

Imethibiti kwa mlolongo wa wapokezi ulio Swahiyh zaidi ya kwamba pindi ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alipomwamrisha Ubayy bin Ka´b kuwaswalisha watu katika swalah Ramadhaan kwa Rak´ah kumi na moja, alikuwa Ubayy (Radhiya Allaahu ´anh) akisoma Aayah mia mbili mpaka wale waliosimama nyuma yake wakitegemea bakora kutokana na urefu wa kisomo. Walikuwa wakibaki katika hali hiyo mpaka mwanzo wa alfajiri[2].

Imesihi pia kutoka kwa ´Umar ya kwamba aliwakusanya wasomaji katika Ramadhaan na akawaamrisha wale wasomao Qur-aan haraka wasome Aayah thelathini, wale wa kati na kati Aayah ishirini na tano na wale wasomao taratibu Aayah ishirini[3].

Kujengea juu ya hili yule anayeswali peke yake anaweza kurefusha anavyotaka. Vivyo hivyo ikiwa amezungukwa na wale wanaokubaliana nae. Kila ambavyo ni ndefu ndivyo inavyokuwa bora zaidi. Lakini hata hivyo asipindukii mpaka akaswali usiku mzima, kitu ambacho kinatakiwa kufanywa mara chache. Badala yake mtu anatakiwa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Uongofu bora ni uongofu wa Muhammad.”[4]

Ama mtu akiwaongoza wengine katika swalah, awarefushie kwa njia isiyowatia uzito wale waswaliji walio nyuma yake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mmoja wenu atapowaswalisha watu, basi aikhafifishe swalah yake. Kwani hakika nyuma yake kuna ambao ni wadogo, wazee, wadhaifu, wagonjwa na wenye haja. Ama akiswali peke yake, basi airefushe swalah yake apendavyo.”[5]

[1] Hadiyth zote hizi ni Swahiyh na zimetajwa katika “Swifat Swalaat-in-Nabiyy”, uk. 117-122.

[2] Ameipokea Maalik na wengineo. Tazama “Swalaat-ut-Taraawiyh”, uk. 52.

[3] Tazama marejeo yaliyotangulia, uk. 71. Vilevile imepokelewa na ´Abdur-Razzaaq katika “al-Muswannaf” (4/621/7731) na al-Bayhaqiy (2/498).

[4] Hiki ni kipande cha Hadiyth iliyopokelewa na Muslim, an-Nasaa´iy na wengineo. Imetajwa katika “Ahkaam-ul-Janaa-iz”, uk. 18, na “al-Irwaa´” (759-760).

[5] al-Bukhaariy na Muslim na nyongeza ni ya Muslim. Imetajwa katika “al-Irwaa´” (512) na “Swahiyh Abiy Daawuud” (759-760).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 25
  • Imechapishwa: 07/05/2019