79. Sharti ya tatu inayomfunguza mfungaji: Matakwa

03 – Awe mwenye kutaka mwenyewe. Kwa maana nyingine ametumia kifunguzi kwa khiyari na matakwa yake mwenyewe. Akiwa amelazimishwa swawm yake ni sahihi na wala halazimiki kulipa. Kwa sababu Allaah (Subhaana) ameondosha hukumu kwa ambaye amekuru kwa kutenzwa nguvu muda wa kuwa moyo wake umetua juu ya imani. Amesema (Ta´ala):

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake – isipokuwa yule aliyetenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu ya imani – lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao wana ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu.”[1]

Kama Allaah amemnyanyulia hukumu ya ukafiri kwa ambaye ametenzwa nguvu juu ya jambo hilo basi aliye chini yake ana haki zaidi ya kunyanyuliwa hukumu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayi  wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah ameusamehe ummah wangu makosa, usahaulifu na yale wanayotenzwa nguvu kwayo.”

Ameipokea Ibn Maajah, al-Bayhaqiy na an-Nawawiy ameifanya kuwa nzuri.

Endapo mume atamtenza nguvu mke wake kufanya tendo la ndoa, ilihali amefunga, basi swawm yake ni sahihi na mwanamke huyo halazimiki kulipa. Si halali kwa mwanamme huyo kumlazimisha tendo la ndoa ilihali amefunga. Isipokuwa ikiwa mwanamke huyo amefunga swawm inayopendeza bila idhini yake ilihali mume wake hakusafiri.

Iwapo vumbi litaruka na kuingia tumboni mwa mfungaji au akaingiwa ndani na kitu kingine pasi na kutaka kwake, au akasukutua au akapalizia ambapo kukateremka tumboni mwake kitu katika maji pasi na kutaka kwake, swawm yake ni sahihi na wala halazimiki kulipa.

[1] 16:106

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 108
  • Imechapishwa: 03/03/2024