79. Nuru pekee ndio hupanda kwa Allaah

Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akapiga mfano wa pili, ambao ni mfano wa moto, na akasema:

وَمِمَّا يُوقِدُونَ عَلَيْهِ فِي النَّارِ ابْتِغَاءَ حِلْيَةٍ أَوْ مَتَاعٍ زَبَدٌ مِّثْلُهُ

”[…] na miongoni mwa wanavyoviwashia moto ili kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vilevile.”[1]

Hii ni kama chuma, shaba, fedha, dhahabu na vinginevyo. Hakika vitu hivi huingizwa katika moto wa tanuru ili visafishwe na kutakaswa na uchafu. Kisha uchafu wake hutoka na hutupwa mbali na kunabaki kilicho safi. Hicho ndicho kinachowanufaisha watu.

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) alipotoa mifano hii miwili, akataja hukumu ya wale waliomuitikia na kufuata uongofu Wake kwa fakhari, na hukumu ya wale wasiomuitikia na ambao hawakufuata uongofu Wake kwa fakhari, akasema:

لِلَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَالَّذِينَ لَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُ لَوْ أَنَّ لَهُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ سُوءُ الْحِسَابِ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمِهَادُ

”Wale waliomuitikia Mola wao watapata mazuri zaidi. Na wale wasiomuitikia – hata kama wangelikuwa wana vyote vilivyomo ardhini na mfano wa kama hivyo pamoja, wangelivitoa kujikombolea navyo. Hao watapata hesabu mbaya na makazi yao ni Jahannam – na ni mahali pabaya mno pa kupumzikia!”[2]

Mkusudio ni kuwa Allaah (Ta´ala) amefanya uhai kuwa mahali palipo nuru na mauti mahali palipo giza. Uhai wa viumbe vyenye roho na viumbe wenye mwili vyote viwili vinategemea nuru, ambayo ndio kiini cha uhai kama ilivyo pia chanzo cha mwangaza. Hakuna uhai bila ya nuru, kama ambavyo hakuna mwangaza bila yake. Kama ambavyo nuru huleta uhai wa moyo, vilevile huleta kuenea kwake, faraja yake na upana wake. at-Tirmidhiy amepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi nuru inapoingia moyoni, basi huenea na kupanuka.” Wakauliza: “Na ni nini alama yake?” Akasema: “Ni kuelekea katika makazi ya kudumu, kujiepusha na makazi ya udanganyifu na kujiandaa kwa kifo kabla ya kufika kwake.”[3]

Nuru ya mja ndio inayopandisha matendo na maneno yake kwa Allaah (Ta´ala). Hakuna kinachopanda Kwake (Ta´ala) isipokuwa maneno mazuri – nayo ni nuru na ina chanzo ndani ya nuru – pamoja na matendo mema na roho nzuri. Hizo ni zile roho za waumini ambazo zinang´aa kwa nuru aliyoiteremsha kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vilevile Malaika, ambao wameumbwa kutokana na nuru, wanayo nuru hiyo. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Malaika wameumbwa kutokana na nuru, majini kutokana na moto na Aadam ameumbwa kwa kile mlichoelezewa.”[4]

Wakati ilipokuwa asili ya Malaika ni kutokana na nuru, basi wao ndio ikawa wanapanda kwa kwa Mola wao (Tabaarak wa Ta´ala). Vivyo hivyo roho za waumini ndizo hupanda kwenda kwa Mola wao wakati wa kutolewa na Malaika. Hufunguliwa milango ya mbingu ya dunia, kisha ya pili, ya tatu, ya nne, mpaka ya saba. Kisha husimamishwa mbele ya Allaah (´Azza wa Jall), kisha huamrishwa kiandikwe kitabu chake kiandikwe miongoni mwa wale wenye cheo cha juu. Wakati ilipokuwa roho hii ni roho safi, nzuri, yenye nuru na mng’a, ndipo ikapaa kwa Allaah (´Azza wa Jall) pamoja na Malaika.

[1] 13:17

[2] 13:18

[3] al-Haakim (4/311), ambaye ameinyamazia.

[4] Muslim (2996).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 143-145
  • Imechapishwa: 27/08/2025