79. Ni Mfalme ndiye anayeshuka chini

78 – Abu Hurayrah amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kunapopita theluthi ya kwanza ya usiku[1], Mola wetu (´Azza wa Jall) hushuka na kusema: ”Mimi ni Mfalme! Ni nani anayeniomba Nimpe? Ni nani ambaye ananiomba Nimuitikie? Ni nani ambaye ananiomba msamaha Nimsamehe?” Huendelea hivo.”[2]

Ameipokea Ahmad na cheni ya wapokezi ni yenye nguvu. Nimeziandika Hadiyth za Ushukaji katika kitabu. Nathibitisha kuwa zimepokelewa kwa mapokezi mengi.

[1] Imekuja katika upokezi mwingine ”wakati kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku”. Hiyo ndio Swahiyh zaidi, kama alivosema at-Tirmidhiy. Tazama ”Irwaa´-ul-Ghaliyl” (450).

[2] Imekuwa ni jambo lililotangaa kwa wale wanaokanusha Ushukaji ya kwamba kilichokusudiwa ni kushuka kwa amri na rehema za Allaah (´Azza wa Jall). Licha ya kwamba tafsiri hii ni batili kwa njia nyingi, kama alivyobainisha Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake ”Sharh Hadiyth-un-Nuzuul”, Hadiyth inatamka waziwazi ya kwamba Allaah (Ta´ala) ndiye anayeshuka pale Anaposema ´Mimi ni Mfalme!`. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Pindi mmoja katika wale viongozi wanaopinga Ujuu waliulizwa kuhusu Ushukaji, akasema ni amri Yake ndio inayoshuka. Wakati muulizaji alipomuuliza inatoka kwa nani ikiwa huko juu hakuna yeyote, anapigwa na butwaa na kunyamaza.” (Sharh Hadiyth-in-Nuzuul, s. 36)

Miongoni mwa tafsiri za ajabu mno nilizoona ni pamoja na maneno ya Shaykh Abu Zahrah, aliyesema:

”Ni sahihi kufasiri Ushukaji katika mbingu ya chini ya kwamba ni kukaribia kwa hesabu Yake (Ta´ala).” (al-Madhaahib al-Ismaamiyyah, uk. 325)

Kutokana na tafsiri hii ni kwamba hesabu ya Allaah inakaribia katika kila usiku! Kwa msemo mwingine ni kwamba hakuna ushukaji kabisa. Namna hii ndivo yanavyokanushwa Maandiko na kupinga maana yake ya kikweli inayolingana na Allaah (Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk. 115-116
  • Imechapishwa: 30/06/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy