79. Mawalii na waja wema hawastahiki chochote katika haki ya Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Pamoja na kwamba hawastahiki chochote katika haki ya Allaah (Ta´ala) na hawaombwi asichokiweza isipokuwa Allaah.

MAELEZO

Pamoja na kwamba hawastahiki chochote katika haki ya Allaah – Huu ni umakini wa mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah). Ndani yake kuna Radd juu ya wale wanaopindukia kwa watu wa karama na wanawaabudu mawalii na waja wema badala ya Allaah kwa madai kwamba wana karama. Hayo yanafanywa na waabudia makaburi ambao wanajikurubisha kwa wafu na wanaitakidi juu ya baadhi ya waliohai ya kwamba wamefikia katika ngazi ambayo wanaweza kuwanusuru na kuwapa vitu ambavyo hakuna aviwezaye isipokuwa Allaah pekee kwa kujengea kwamba anazo karama. Wanasema kuwa anazo karama na kwamba hiyo ni dalili ya kuonyesha kuwa ananufaisha na anadhuru. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anawaraddi watu hawa. Mara nyingi yale yanayofanywa na waabudia makaburi yamejengeka juu ya dhana hii; kuchupa mpaka juu ya watu wenye karama.

Sisi  tunawapenda waja wema na wale ambao mikononi mwao kunafanyika karama. Tunawapenda, tunawatukuza na tunawaigiliza. Lakini hatuwapi kitu katika ´ibaadah kama wanavofanya makhurafi.

Maneno yake:

“…katika haki ya Allaah (Ta´ala).”

Haki ya Allaah ni ´ibaadah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Haki ya Allaah juu ya waja wamwabudu Yeye na wasimshirikishe na chochote.”[1]

Maneno yake:

“… hawaombwi asichokiweza isipokuwa Allaah.”

Kwa mfano wa kuleta riziki, kumponya mgonjwa, kumpa mtu mtoto na mengineyo. Haya hakuna ayawezaye isipokuwa Allaah. Kuhusu yale wanayoyaweza katika mambo ya kidunia wanaombwa midhali wako hai. Haijalishi kitu hata kama hawana karama. Unaweza kumuona mtu akusaidie mali. Kwa mfano ni tajiri na ukamuomba akukope au akupe swadaqah. Ukitumbukia katika janga unamuomba akusaidie kuondoka ndani yake. Imekuja katika Hadiyth:

“Ambaye yuko katika haja ya ndugu yake basi Allaah anakuwa katika haja yake. Mwenye kumwondoshea muislamu tatizo, basi Allaah atamwondoshea tatizo miongoni mwa matatizo ya siku ya Qiyaamah.”[2]

Kwa hivyo inafaa kuwataka msaada viumbe waliohai katika yale mambo wanayoyaweza. Amesema (Ta´ala):

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ

“Akamsaidia yule ambaye ni katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake, Muusa akampiga ngumi akamuua.”[3]

Mmoja katika wana wa israaiyl alimtaka msaada Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) dhidi ya mmoja katika jamaa zake Fir´awn ambapo Muusa akamsaidia mtu huyu mwenye kudhulumiwa. Vilevile ni kama ambavo mtu anawataka msaada wenzake vitabu na venginevyo. Hakuna ubaya wowote mtu akawataka msaada wenzake katika yale wayawezayo. Amesema (Ta´ala):

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖوَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

“Saidiane katika wema na kumcha Allaah na wala msisaidiane katika dhambi na uadui.”[4]

[1] al-Bukhaariy (2856) na Muslim (30) kupitia kwa Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] al-Bukhaariy (2442) na Muslim (2580) kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[3] 38:15

[4] 05:02

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 114-115
  • Imechapishwa: 24/05/2021