Swali 78: Nyinyi na ndugu zako wanazuoni wa nchini ni Salafiyyuun. Mnawanasihi watawala kwa njia iliyowekwa katika Shari´ah aliyoibainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo kuna watu wanaokulaumuni kwamba hamkemei madhambi yanayofanywa hadharani. Wengine wanakupeni udhuru na kusema kuwa mnashinikizwa na nchi. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Hapana shaka kuwa watawala ni kama wanadamu wengine wote, hawakukingwa na makosa. Ni wajibu kuwanasihi[1]. Lakini kuwanyanyasa katika vikao na katika mimbari ni usengenyi ulioharamishwa[2]. Dhambi hiyo ni kubwa kuliko ile inayofanywa na watawala, kwa sababu ni usengenyi. Usengenyi huo unapelekea katika mitihani na mfarakano na kuathiri ulinganizi[3]. Ni lazima kuwanasihi kwa njia ya amani na si kwa njia kuwafedhehesha.

[1] Ibn Abiy ´Aaswim amesema:

”Mlango unaozungumzia wananchi wanapaswa kuwanasihi watawala wao.  Zayd bin Thaabit (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Moyo wa muislamu hauingiwi na vifundo juu ya mambo matatu: kumtakasia matendo Allaah, kuwanasihi watawala na kulazimiana na mkusanyiko. Kwa sababu du´aa yao inawazunguka wengine wote.” (as-Sunnah (2/502))

al-Albaaniy amesema kuwa cheni ya wapokezi ni Swahiyh.

[2] Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:

”Ama kuwatukana viongozi juu ya mimbari sio ufumbuzi. Ufumbuzi ni kuwaombea du´aa ya uongofu, kuwafikishwa, kutengemaa kwa nia na kutengemaa kwa wale marafiki. Hii ndio suluhu. Kwa sababu kuwatukana hakuwazidishii kheri yoyote. Kuwatukana sio katika manufaa. Kuwatukana na kuwalaani sio katika Uislamu.” (Fataawaa al-´Ulamaa’ al-Kibaar, uk. 65, ya ´Abdul-Maalik Ramadhwaaniy)

[3] Pia inapelekea wao kutotiiwa, kutosikizwa katika yaliyo mema na kumwagika kwa damu. ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) aliuliwa kwa sababu ya makemeo ya waziwazi yaliyozuliwa na Khawaarij.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 195-200
  • Imechapishwa: 21/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy