Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

65 – Imani ya mtu juu ya kuonekana [kwa Allaah] kwa watu wa Peponi haisihi ikiwa mtu atazingatia hilo kwa kupindisha maana. Kwa sababu kila maana, kukiwemo Kuonekana, ambayo inaegemezwa kwa Mola haitakiwi kupindishwa maana na badala yake mtu alazimiane na kujisalimisha. Hiyo ndio dini ya waislamu.

MAELEZO

Imani ya mtu kuamini watu wa Peponi kumuona Allaah haisihi ikiwa mtu analipindishia maana au kulifasiri kwa dhana mbovu na akakanusha uhakika wake na asijisalimishe kwa Allaah wala kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaliingilia kwa fikira na fahamu yake.

Yote haya ni kuzidi kutilia mkazo yale yaliyotangulia kwamba ni lazima kujisalimisha kwa yale yote yaliyokuja kutoka kwa Allaah na kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Miongoni mwa mambo hayo ni Kuonekana. Hatulipekui kama walivyofanya Ahl-ul-Bid´ah. Bali tunalithibitisha kama lilivyokuja na kuliamini. Tunathibitisha kuwa waumini watamuona Mola wao katika Uwanja wa siku ya Qiyaamah kabla ya kuingia kwao Peponi, na pia baada ya kuingia kwao Peponi. Hivo ndivo Allaah atavyowakirimu kwa vile walimuamini duniani ilihali hawajamuona. Hii ndio dini ya waislamu. Wanaamini na kujisalimisha kwa yale yote yaliyokuja kutoka kwa Allaah na kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kulipekua kwa fahamu mbovu, tafsiri mbovu na upotoshaji wa maana. Huu ndio Uislamu tofauti na dini nyenginezo ambazo wafuasi wake wanayapekua yale yenye kutoka kwa Allaah na yenye kutoka kwa Mtume Wake na wanakengeusha maneno yao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 23/01/2023