Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotulia al-Madiynah, alifaradhishiwa Shari´ah zingine za Kiislamu. Kwa mfano zakaah, swawm, hajj, adhaana, jihaad, kuamrisha mema na kukataza maovu na Shari´ah zingine za Kiislamu.

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifaradhishiwa Shari´ah zingine za Kiislamu baada ya kutulizana al-Madiynah an-Nabawiyyah. Makkah alifanya karibu miaka kumi akilingania katika Tawhiyd tu. Baada ya hapo ndio akafaradhishiwa swalah tano Makkah. Kisha akahajiri kwenda al-Madiynah na hakufaradhishiwa zakaah, swawm, hajj wala ´ibaadah nyenginezo katika mambo ya Kiislamu. Dhahiri ya maneno ya mtunzi (Rahimahu Allaah) yanaashiria kwamba zakaah ilifaradhishwa kikamilifu al-Madiynah. Hata hivyo baadhi ya wanachuoni wamesema kuwa zakaah ilifaradhishwa kwanza Makkah. Hata hivyo viwango vya masharti yake vilikuwa havijulikani kama jinsi bidhaa inayowajibika kulipiwa pia ilikuwa haijulikani. Viwango viliwekwa al-Madiynah kwanza na bidhaa iliyo ya wajibu ikawekwa pia. Wametumia dalili ya Aayah za Suurah za Makkah zinazowajibisha zakaah. Mfano mfano wa maneno Yake (Ta´ala) katika Suurah “al-An´aam”:

وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

“Toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake.” (al-An´aam 06 : 141)

وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَّعْلُومٌ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ

”Na wale ambao katika mali zao wana fungu maalum, kwa ajili ya muombaji na aliyenyimwa.” (al-Ma´aarij 70 : 24-25)

Kwa hali yoyote maoni yaliyo sahihi ni kwamba, kuwekwa kwa zakaah, viwango vyake, bidhaa zake za wajibu na aina ya watu wanayoistahiki ilikuwa ni al-Madiynah. Vivyo hivyo adhaana na swalah ya ijumaa. Lililo la dhahiri ni kwamba swalah ya mkusanyiko ilifaradhishwa pia al-Madiynah, kwa sababu adhaana inayowaita watu katika swalah ya mkusanyiko ilifaradhishwa mwaka wa pili baada ya Hijrah. Ama zakaah na swawm vilifaradhishwa mwaka wa tatu baada ya Hijrah. Kuhusiana na hajj ilifaradhishwa mwaka wa tisa baada ya Hijrah kwa mujibu wa maoni yenye nguvu ya wanachuoni. Hapo ilikuwa wakati ambapo Makkah ilikuwa umeshakuwa mji wa Kiislamu, baada ya kutekwa katika mwaka wa tisa baada ya Hijrah. Hali kadhalika kuamrisha mema, kukataza maovu na mengineyo katika zile nembo zilizodhahiri zilizoteremshwa. Yote yalifaradhishwa al-Madiynah baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutulia ndani yake na kusimamisha nchi ya Kiislamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 140-141
  • Imechapishwa: 03/06/2020