76. Mitume walikuwa wakimuonyesha Allaah huzuni wao

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anampa mtihani mja Wake ili kusikia malalamiko yake, kunyenyekea kwake Kwake, kumuomba na kusubiri na kuridhia hukumu Yake. Allaah (Subhaanah) anawaona waja Wake pindi anapopanga kitu cha kuwajaribia. Anajua hali ya kila mmoja. Anamlipa kila mja kwa kusudio na nia yake. Allaah amewasema vibaya wale wasiomnyenyekea na wasiomuomba wakati wanapofikwa na majanga:

وَلَقَدْ أَخَذْنَاهُم بِالْعَذَابِ فَمَا اسْتَكَانُوا لِرَبِّهِمْ وَمَا يَتَضَرَّعُونَ

“Hakika Tuliwachukua kwa adhabu, basi hawakunyenyekea kwa Mola wao na wala hawatoomba rehema.” 23:76

Mja ni dhaifu kabisa kwa yeye kuwa imara mbele ya Mola wake na asimlalamikie. Allaah amewasifu viongozi wa viumbe, ambao ni Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) waliokingwa na kukosea, kwa wao kumshtakia Allaah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema kuhusu baadhi yao:

وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ

“Dhan-Nuun alipoondoka [kwenda baharini] akiwa ameghadhibika akadhani kwamba Hatuna mamlaka juu yake. [Alipopata adhabu yake] akaita katika kiza: “Hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe! Utakasifu ni Wako! Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.” 21:87

Amemsifu Ayyuub na kusema:

وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ

“Na Ayyuub alipomwita Mola wake: “Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe ndiye mbora kabisa wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu.” 21:83

Amemsifu Ya´quub na kusema:

إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Hakika mimi machozi na huzuni wangu namshitakia Allaah na najua kutoka kwa Allaah kitu msichokijua.” 12:86

Amemsifu Muusa na kusema:

رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ

“Mola wangu! Hakika mimi ni mhitajia mkubwa wa kheri Utakayoniteremshia!” 28:24

Kumshtakia Allaah (Ta´ala) hakupingani na subira wala ridhaa. Bali ni katika ujinga wa mja juu ya Muumba wake badala yake kumshtakia mwengine. Hiyo ina maana kwamba hayuko radhi na Muumba wake na hana subira juu ya yale Allaah aliyomjaribu kwayo. Allaah anamchukia yule mwenye kumshtaki kwa waja Wake na anampenda yule mwenye kumshtakia Yeye.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 169-170
  • Imechapishwa: 16/11/2016