Swali 74: Hivi sasa kumeenea jambo la kuwatukana wanazuoni wakubwa na kuwarushia tuhuma za kufuru na ufuska. Hilo khaswa baada ya kutoa fataawaa zao kuhusu kujilipua na kwamba wanazuoni hao wana unyonge katika kupenda na kuchukia kwa ajili ya Allaah. Ni ipi hukumu ya kuwaraddi vijana wanaosema hivo?

Jibu: Mjinga asizungumze. Anapaswa kunyamaza na kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na asizungumze pasi na elimu. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika si vyenginevyo Mola wangu ameharamisha machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [aina zote] na ukandamizaji bila ya haki na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa ambayo hakukiteremshia mamlaka na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[1]

Haijuzu kwa mjinga kuzungumza katika mambo ya kielimu na khaswa mambo makubwa kama vile ya Takfiyr.

Isitoshe kitendo hicho ni usengenyi, umbea na kuzikiuka heshima za watawala na wanazuoni[2]. Hii ni ndio aina mbaya kabisa ya usengenyi. Jambo hili halijuzu.

Mambo haya na mfano wake yanashughulikiwa na watu wa mamlaka. Wao ndio wanayatafiti na kushauriana kwayo. Yanashughulikiwa na wanazuoni wanazuoni. Wao ndio ambao wanabainisha hukumu yake kwa mujibu wa Shari´ah. Kuhusu watu wa kawaida, wajinga na wanaoanza hawatakiwi kuingia katika mambo kama hayo. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَإِذَا جَاءَهُمْ أَمْرٌ مِّنَ الْأَمْنِ أَوِ الْخَوْفِ أَذَاعُوا بِهِ ۖ وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنبِطُونَهُ مِنْهُمْ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَاتَّبَعْتُمُ الشَّيْطَانَ إِلَّا قَلِيلًا

“Linapowafikia jambo lolote la amani au la khofu huharakia kulitangaza. Na lau wangelirudisha kwa Mtume na kwa wale wenye madaraka kati yao, basi wale wanaotafiti miongoni mwao wangelilijua. Lau si fadhilah za Allaah juu yenu na rehema Zake, basi hakika mngelimfuata shaytwaan isipokuwa wachache tu.” [3]

Ni lazima kijizuia ulimi kuongea mambo kama haya, khaswa jambo la kukufurisha na kupenda na kuchukia kwa ajili ya Allaah. Mtu anaweza kuwahukumu watu upotofu na kufuru ilihali amekosea. Katika hali hiyo hukumu inamrejelea yeye. Kwa sababu mtu akimwambia nduguye kuwa ni kafiri au fasiki na mambo sivyo, basi hukumu hiyo inamrudilia yeye[4].

Jambo ni la khatari sana. Ni lazima kwa kila anayemcha Allaah auzuie ulimi wake isipokuwa wale ambao wanastahiki na wamepewa kazi hiyo, kwa mfano watawala na wanazuoni. Ama watu wa kawaida na wanafunzi wadogo hawana haki ya kutoa fatwa, kuwahukumu watu na kuzikiuka heshima za watu. Ni wajinga, wanasengenya, wanaeneza umbea na wanazungumza ni nani ambaye ni kafiri na ni nani ambaye ni mtenda dhambi. Yote haya yanawarejelea. Hayamdhuru wale walengwa, bali yanawarejelea wao. Ni wajibu kwa muislamu kuzuia ulimi wake na wala asiingilie jambo lisilomuhusu[5]. Ama kuzipekua hukumu za Shari´ah, akahukumu ni nani amepatia na ni nani amekosea, akazikiuka heshima za watawala na heshima za wanazuoni na akawahukumu ukafiri au upotofu, ni jambo la khatari kubwa kwa mtu huyo. Wale walengwa hawadhuriki na maneno yake.

Elimu inapotea kwa kufariki wanazuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah hatoiondoa elimu hii kwa kuinyakua kutoka kwenye vifua vya wanazuoni, lakini ataiondoa elimu kwa kufa kwa wanazuoni, mpaka pasibakie mwanachuoni yoyote ndipo watu watawachukua viongozi wajinga. Watawauliza maswali wafutu bila ya elimu. Matokeo yake watapotea na kuwapoteza wengine.”[6]

Naapa kwa Allaah hii ndio hali ya leo. Hivi sasa viongozi wajinga ndio ambao wanazungumzia hukumu za Shari´ah, wanawaelekeza watu, wanatoa mihadhara na wanatoa Khutbah ilihali hawana chochote katika elimu wala ufahamu. Hakuna walicho nacho isipokuwa masaha na mihemko. Wanajishughulisha watu na porojo. Haya yanathibitisha yale aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba watu watawafanya wajinga kuwa ndio viongozi wao[7]. Kwa masikitiko makubwa watu wanaiwaita kuwa ni ” wanazuoni”. Sambamba na hilo hawawezi kujibu jawabu sahihi endapo utawauliza mambo ya kisasa au hukumu za Kishari´ah. Kwa sababu kwa mujibu wanaona kuwa hii sio elimu. Kwa mujibu wao elimu ni zile tamaduni za kisiasa na kuyaelewa mambo ya kisasa. Kwa ajili hiyo ndio maana wakanyimwa elimu.

[1] 7:33

[2] Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh amesema:

”Ni wajibu kwa kila muumini ajihadhari sana kuzungumza pasi na elimu na kufanya ujasiri wa kujiingiza ndani ya mambo wasiyokuwa na hoja kwayo. Hili khaswa katika mambo ya ´Aqiydah, imani, Takfiyr, ya halali na ya haramu… Miongoni mwa upotofu mkubwa uliotokea katika ummah ni kuwakufurisha waislamu… Katika zama za ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) ndipo walijitokeza Khawaarij hawa. Msingi wa kupinda kwao ni kwamba waliona kuwa ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) hakutekeleza yale aliyomuwajibishia Allaah. Miongoni mwao wako ambao walimkufurisha, wengine wakaona kuwa ni wajibu kumuua… wakamkufurisha ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh). Vivyo hivyo watu bora wa ummah walikufurishwa na wale wapinzani wao… Takfiyr maana yake ni kumhukumu mtu kutoka katika dini na kumhukumu kuritadi… Kumhukumu kuritadi muislamu ambaye umethibiti Uislamu wake haijuzu isipokuwa kwa dalili inayokubalika kwa mujibu wa Shari´ah na yenye yakini kama ambavo imani yake ilivyothibiti kwa mujibu wa dalili yenye yakini. Tuhuma kwamba wanazuoni wakubwa ni makafiri ni jambo la khatari mno. Kwa sababu wanazuoni wakubwa wanaibainisha haki. Mtu akiwatuhumu au akawarushia ukafiri kwa sababu ya kubainisha kwao haki, haina maana kuwa tuhuma za mwenye kutuhumu zinaafikiana na usawa. Bali mtuhumu ameifanyia vibaya nafsi yake mwenyewe. Mtu kama huyo anatakiwa kuadhibiwa na mahakamana… Na licha ya kwamba maudhui haya yalifanyiwa utafiti kuanzia hapo kitambo mpaka hivi sasa na wanazuoni kama vile Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz na Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn (Rahimahumaa Allaah), lakini tunachelea kuwa mfumo wa kuwakufurisha watu umekuwa ni wenye kuenea kati ya watu na kwamba Khawaarij na fikira zao bado zitaendelea. Watu wanaweza kuwa na sifa miongoni mwa sifa za wapotofu wasipojihadhari kutokana na hilo. Kwa ajili hiyo ni wajibu kwetu sote tujihadhari na tuzinduke juu ya haki na tuhimizane juu yake na tuzilinde ndimi zetu kutokana na kuwatukana wanazuoni, ambao ndio warithi wa Mitume.” (al-Fataawaa al-Muhimmah fiy Tabswiyr-il-Ummah, uk. 49-61)

[3] 04:83

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuamrisha mema na kukataza maovu kunatakiwa kuwa kwa urafiki. Ndio maana ikasemwa kitendo cha mmoja kuamrisha mema kinatakiwa iwe wema na kukataza maovu isiwe maovu. Ikiwa kuamrisha mema na kukataza maovu ni katika mambo ya wajibu makubwa au yanayopendeza, basi ni lazima manufaa yawe makubwa zaidi kuliko madhara… Yote ambayo Allaah ameamrisha ni mazuri. Allaah amesifia wema na watengenezaji na akasema vibaya maharibifu na wenye kuharibu maeneo mengi. Ikiwa madhara ya kuamrisha au kukataza ni makubwa zaidi kuliko manufaa, basi sio kitu ambacho Allaah ameamrisha hata kama kutaachwa jambo la wajibu au kukafanywa jambo la haramu. Kwani muumini anatakiwa kumcha Allaah kutokana na waja wa Allaah. Yeye kazi yake sio kuwaongoza.” (al-Amr bil-Ma´ruuf wan-Nahiy ´an-il-Munkar, uk. 19)

[4] al-Bukhaariy (5753).

[5] Badala yake mtu anatakiwa kujitahidi kuitafuta elimu ya Shari´ah ambayo ndio uhai wa moyo na inayomnyanyua mja duniani na Aakhirah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

“Allaah atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu. Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mjuzi wa ndani kabisa.” (58:11)

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote mwenye kushika njia akitafuta kwayo elimu, basi Allaah atamsahilishia njia ya kuelekea Peponi.” (Muslim (2699))

Elimu inamzuia mwenye nayo kuingia katika mambo yanayopingana na dini, kufuata matamanio na njia ya shaytwaan. Ibn-ul-Qaasim amesimulia kuwa amemsikia Imaam Maalik akisema:

”Kikosi cha watu wanajibidisha na ´ibaadah na wakaiacha elimu. Matokeo yake wakawafanyia uasi ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa panga zao. Endapo wangelitafuta elimu basi wasingeyafanya hayo.”

Ibn Wahb amesema:

”Nilikuwa kwa Maalik bin Anas ambapo nikasimama na kuanza kuswali. Ndipo akasema: ”Hakikuwa kile ulichosimama kwa ajili yake bora kushinda kile ulichokiacha.” (Miftaah Daar-is-Sa´aadah (1/119-120))

Bi maana elimu.

Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Lazimianeni na elimu. Kwani hakika kujifunza nayo ni ´ibaadah, kuifunza kwa ajili ya Allaah ni tendo jema, kuitoa kwa wenye nayo ni kujikurubisha, kumfunza nayo yule asiyeijua ni swadaqah, kuitafuta ni jihaad na kujikumbusha nayo ni kutukuza.” (ad-Daylamiy (1/41) na Majmuu´-ul-Fataawaa (4/42) ya Ibn Taymiyyah)

[6] al-Bukhaariy (100).

[7] Kuna daktari mmoja katika Sunnah amesema:

”Naanza wapi? Naanza vipi? Ee damu, nisaidie! Ee moyo wangu, simama nami! Ee damu, niokoe!”

Hii ndio hali yao ya ujinga na mkanganyiko. Vinginevyo ukimuuliza mmoja katika wanafunzi wetu wa shule za msingi ni nani anayetakiwa kumuomba na kumtaka msaada na kumtaka uokozi wakati wa matatizo na shida, atajibu kwa kusema ”Allaah”. Watu wana haja kubwa kiasi gani kuijua, kujifunza na kuifahamu Tawhiyd! Haja inakuwa kubwa zaidi kwa mfano wa watu kama hawa ambao wamejiteua wao wenyewe kuwa ni viongozi, walezi na walinganizi. Lakini ni vipi watakuwa na hamu ya kuwafunza watu Tawhiyd ilihali kalima na mihadhara yao inadharau Tawhiyd na kuifanya si jambo jepesi na badala yake nguvu kubwa wameitia katika siasa? Amekwishatangulia mmoja katika watu hawa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 186-191
  • Imechapishwa: 14/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy