74. Baadhi ya Adhkaar mwishoni mwa swalah na baada ya swalah

Swali 74: Ni yepi makusudio ya (بدبر الصلاة) katika zile Hadiyth ambazo kumepokelewa ndani yake mahimizo ya kuomba du´aa au Dhikr بدبر ya kila swalah? Je, ni pale mwishoni mwa swalah au ni baada ya salamu?

Jibu: Neno بدبر husemwa kwa kuachiwa mwishoni mwake kabla ya salamu na wakati mwingine husemwa kwa kuachiwa kukakusudiwa moja kwa moja baada ya salamu. Sentesi hiyo imepokelewa katika Hadiyth ambazo ni Swahiyh na nyingi katika hizo zinafahamisha kuwa makusudio ni mwishoni mwake kabla ya salamu kwa yale yanayohusiana na du´aa. Baadhi yake ni Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimfunza Tashahhud kisha akasema:

“Kisha achague katika du´aa inayompendeza aiombe.”

Imekuja katika tamko jingine:

“Kisha achague katika mahitaji anayotaka.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Miongoni mwa hayo ni Hadiyth ya Mu´aadh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia: “Usiache دبر kila swalah kusema:

اللّهُـمَّ أَعِـنِّي عَلـى ذِكْـرِكَ وَشُكْـرِك وَحُسْـنِ عِبـادَتِـك

“Ee Allaah! Nisaidie juu ya kukutaja, kukushukuru na kufanya vyema katika kukuabudu.”

Ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa´iy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Miongoni mwa hayo ni yale aliyopokea al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) kupitia kwa Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema دبر ya kila swalah:

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَعوذُ بِكَ مِنَ البُخْـل، وَأَعوذُ بِكَ مِنَ الجُـبْن، وَأَعوذُ بِكَ مِنْ أَنْ أُرَدَّ إِلى أَرْذَلِ الـعُمُر، وَأَعوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَـةِ الدُّنْـيا وَعَـذابِ القَـبْر

”Ee Allaah najikinga Kwako kutokamana na ubakhili, najikinga Kwako kutokamana na woga, najikinga Kwako kutokamana na kurudishwa katika umri duni, najikinga Kwako kutokamana na fitina ya dunia na adhabu ya kaburi.”

Kuhusu Adhkaar zilizopokelewa juu ya hilo zimefahamisha Hadiyth Swahiyh juu ya kwamba zinasemwa دبر ya swalah baada ya salamu. Miongoni mwa hayo ni yeye aseme baada ya kutoa salamu:

أَسْـتَغْفِرُ الله، أَسْـتَغْفِرُ الله، أَسْـتَغْفِرُ الله، اللّهُـمَّ أَنْـتَ السَّلامُ، وَمِـنْكَ السَّلام، تَبارَكْتَ يا ذا الجَـلالِ وَالإِكْـرام

”Namuomba Allaah msamaha, namuomba Allaah msamaha,  namuomba Allaah msamaha. Ee Allaah! Wewe ndiye as-Salaam na amani inatoka Kwako na umetukuka, Ee Mwenye utukufu na ukarimu.”

Ni mamoja ni imamu, maamuma au anayeswali peke yake. Baada ya hapo imamu atawageukia waswaliji na kuwaelekezea uso wake na imamu, maamuma na anayeswali peke yake watasema baada ya kumaliza kusema Dhikr hii na kuleta Istighfaar:

لا إله إلا الله، وحده لا شريك له، له الملك، وله الحمد، وهو على كل شيء قدير، لا حول ولا قوة إلا بالله، لا إله إلا الله، ولا نعبد إلا إياه، له النعمة وله الفضل وله الثناء الحسن، لا إله إلا الله مخلصين له الدين ولو كره الكافرون. اللهم لا مانع لما أعطيت ولا معطي لما منعت ولا ينفع ذا الجد منك الجد

“Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, ufalme ni Wake na himdi zote njema ni Zake na Yeye juu ya kila jambo ni muweza.  Hapana uwezo wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, wala hatumwabudu mwengine isipokuwa Yeye, ni Zake neema, fadhilah ni Zake na ni Zake sifa zote nzuri, hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kumtakasia Yeye dini, ijapokuwa watachukia makafiri. Ee Allaah! Hakuna awezaye kuzuia ulichokitoa na wala kutoa ulichokizuia na wala utajiri wa mtu haumnufaishi mwenye utajiri mbele Yako.”

Inapendeza kwa muislamu wa kiume na muislamu wa kike kusema Dhikr hii baada ya zile swalah zote tano. Baada ya hapo alete Tasbiyh, Tahmiyd na Takbiyr mara thelathini na tatu kisha aseme hali ya kukamilisha mia moja:

لا إله إلا الله، وحده لا شريك له، له الملك، وله الحمد، وهو على كل شيء قدير

“Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, ufalme ni Wake na himdi zote njema ni Zake na Yeye juu ya kila jambo ni muweza.”

Kumethibiti Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya yote haya. Baada ya haya inapendeza kusoma kimyakimya Aayah “al-Kursiy” mara moja na asome:

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيم. قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

”Kwa jina la Allaah, Mwingi wa kurehemu, Mwenye kurehemu. Sema: ”Allaah ni Mmoja pekee, Mwenye kutegemewa kwa haja zote, hakuzaa na wala hakuzaliwa na wala haiwi awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye.”

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ .قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَق مِن شَرِّ مَا خَلَقَ وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ  وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ

”Kwa jina la Allaah, Mwingi wa kurehemu, Mwenye kurehemu. Sema: ”Najilinda na Mola wa mapambazuko, kutokamana na shari ya alivyoviumba, na kutokamana na shari ya giza linapoingia, kutokamana na shari ya wapulizao mafundoni na kutokamana na shari ya hasidi anapohusudu.”

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ .قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ مَلِكِ النَّاسِ إِلَـٰهِ النَّاسِ مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ

”Kwa jina la Allaah, Mwingi wa kurehemu, Mwenye kurehemu. Sema: ”Najilinda na Mola wa watu, mfalme wa watu, mwabudiwa wa haki wa watu, kutokamana na shari za anayetia wasiwasi, mwenye kurejea nyuma, anayetia wasiwasi nyoyoni mwa watu miongoni mwa majini na watu.”

mara mojamoja baada ya kila swalah kimyakimya. Isipokuwa katika Maghrib na Fajr inapendeza kwake kukariri Suurah hizi tatu zilizotajwa mara tatutatu.

Vilevile inapendeza kwa muislamu wa kiume na muislamu wa kike baada ya swalah ya Maghrib na Fajr kusema:

لا إله إلا الله وحده لا شريك له له الملك وله الحمد يحيي ويميت وهو على كل شيء قدير

“Allaah ni mkubwa. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Ufalme ni Wake Yeye na himdi zote ni Zake Yeye. Anahuisha na Anafisha. Naye juu ya kila jambo ni muweza.”

mara kumi kwa kuongezea yale yaliyokwishatangulia kabla ya kusoma Aayah ya “al-Kursiy” na kabla ya kusoma Suurah tatu kwa ajili ya kutendea kazi Hadiyth Swahiyh zilizopokelewa juu ya hilo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 76-80
  • Imechapishwa: 20/09/2022