73. Mwenye kukanusha Tawhiyd ni kafiri wa kupindukia kuliko anayekanusha uwajibu wa swalah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Inaweza pia kusemwa: Ikiwa unathibitisha ya kwamba yule ambaye anamsadikisha Mtume katika kila kitu na akakadhibisha uwajibu wa swalah, ni kafiri ambaye ni halali kumwagwa damu yake kwa maafikiano, hali kadhalika akikubali kila kitu isipokuwa kufufuliwa, hali kadhalika lau atakadhibisha uwajibu wa kufunga swawm ya Ramadhaan, hakanushi isipokuwa haya peke yake ilihali mengine yote anayasadikisha – madhehebu mbalimbali wamekubaliana kwa hili na Qur-aan imeliongelea kama tulivyosema – mtu atafahamu [elewa] ya kwamba Tawhiyd ndio faradhi kubwa aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ndio [wajibu] mkubwa kuliko swalah, zakaah, swawm na hajj. Vipi basi itakuwa mtu akikadhibisha kitu katika mambo haya anakufuru – hata kama atayafanyia kazi mambo yote aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na akikadhibisha [pinga] Tawhiyd ambayo ni dini ya Mitume wote asikufuru. Ametakasika Allaah! Ni ajabu ilioje ya ujinga huu!

MAELEZO

Hili ni jibu la pili. Ni vipi unaweza kupinga yule mwenye kukanusha Tawhiyd na akamshirikisha Allaah hawi kafiri, ilihali unatambua na kukubali ya kwamba mwenye kukanusha swalah, zakaah, swawm, hajj na kufufuliwa anakuwa kafiri? Hili ni jambo la ajabu kwelikweli pale unapoona mwenye kukanusha Tawhiyd ni muislamu, wakati unaona mwenye kukanusha uwajibu wa mambo haya anakuwa kafiri! Pamoja na kuwa Tawhiyd ndio jambo kubwa walilokuja nalo Mitume (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam). Ndio jambo lililoenea walilotumwa nalo Mitume. Mitume wote walitumwa nalo. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Na Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi Niabuduni.”” (21:25)

Tawhiyd ndio msingi wa mambo haya ya wajibu, kwa sababu hayasihi isipokuwa kwayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ

“Kwa hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako [kwamba]: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika. Bali Allaah mwabudu pekee na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.” (39:65-66)

Ikiwa yule mwenye kupinga uwajibu wa swalah, zakaah, swawm na hajj na kufufuliwa ni kafiri, basi mwenye kukanusha Tawhiyd ni kafiri wa kipindukia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 84
  • Imechapishwa: 25/11/2023