73. Hadiyth ”Tumeamrishwa kukuswalia na kukutakia amani… ”

73 – Naswr bin ´Aliy ametuhadithia: ´Abdul-A´laa ametuhadithia: Hishaam ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan bin Bishr bin Mas´uud, ambaye ameeleza:

”Tulisema – au kulisemwa kuambiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Tumeamrishwa kukuswalia na kukutakia amani. Kuhusu kukutakia amani tumekwishajua, lakini ni vipi tunakuswalia?” Akasema: ”Semeni:

اللهم صل على آل محمد، كما صليت على آل إبراهيم، اللهم بارك على محمد، كما باركت على آل إبراهيم

”Ee Allaah! Wasifu jamaa zake Muhammad kama Ulivyowasifu jamaa zake Ibraahiym. Ee Allaah! Mbariki Muhammad kama Ulivyowabariki jamaa zake Ibraahiym.”[1]

[1] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kama ile ilio kabla yake. Lakini ameipokea an-Nasaa´iy kupitia kwa ´Abdul-Wahhaab bin ´Abdil-Hamiyd, kutoka kwa Hishaam bin Hassaan, isipokuwa tu tofauti ni kwamba ameisimulia kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin Bishr, kutoka kwa Abu Mas´uud al-Answaariy, aliyesema:

”Kulisemwa kuambiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… ”

Cheni ya wapokezi wake iko na Ibn Bishr, kutoka kwa Abu Mas´uud al-Answaariy. Pengine alikosea kwa ´Abdul-Wahhaab bin ´Abdil-Hamiyd. Hata kama alikuwa mwaminifu, kumbukumbu yake ilibadilika miaka mitati kabla ya kufa kwake. Upokezi wa sawa ni kupitia kwa ´Abdul-A´laa bin ´Abdil-A´laa al-Baswriy as-Saamiy, kutoka kwa Hishaam, kwa sababu unaafikiana na upokezi wa Ibn ´Awn, Ayyuub na wa Muhammad bin Siyriyn. Vilevile Hadiyth imepokelewa kupitia njia nyingine iliyoungana kutoka kwa Ibn Mas´uud. Imekwishatangulia katika kitabu (63).

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Ishaaq al-Maalikiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-us-Swalaah ´alaan-Nabiy, uk. 68
  • Imechapishwa: 04/02/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy