72. Radd juu ya utata wa kumi na tatu: kujuzu kuwaomba maiti kwa kuwa Jibriyl alitaka kumsaidia Ibraahiym (صَلَّى اللّٰهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)

Wana shubuha nyingine. Nayo ni kisa cha Ibraahiym alipotumbukizwa kwenye moto, Jibriyl akamfunulia na kusema: “Je, una haja ya kitu?” Akasema Ibraahiym: “Ama kama ni kutoka kwako, hapana.” Wanasema: “Lau kama kuombwa msaada Jibriyl ni shirki, basi asingejionesha kwa Ibraahiym.” Jibu ni: “Kwa hakika hii ni kama ile shubuha ya kwanza. Kwa hakika Jibriyl alijionyesha kwake ili kumnufaisha kwa kitu ambacho anakiweza, kwani hakika yeye ni kama Allaah alivyomzungumza:

شَدِيدُ الْقُوَىٰ

”Mwenye nguvu kwelikweli.” (an-Najm 53 : 05)

Lau Allaah angelimruhusu kuchukua moto wa Ibraahiym, ardhi na milima na kuvitupa mashariki au magharibi, angelifanya hivyo. Na lau Alingelimuamrisha kumuweka Ibraahiym (´alayhis-Salaam) mahali ambapo ni mbali na wao, angelifanya hivyo. Na lau Angelimuamrisha kumpandisha mbinguni, angalifanya. Hili ni kama mfano wa mtu tajiri ana mali nyingi na ameona mtu mwenye kuhitajia. Akajitolea kumpa mkopo au kumpa kitu atatue kwazo haja yake. Lakini yule mwenye kuhitajia akakataa kuzichukua na akasubiria Allaah kumpa riziki yake mwenyewe. Hili lina mafungamano yepi na kuomba msaada wa ki-´Ibaadah na shirki, lau wangelikuwa wanafahamu?

MAELEZO

Huu ni utata wa mwisho uliyotajwa na Shaykh katika kitabu hiki kikubwa. Ameujibu kwa jibu ambalo ni zuri sana. Nao ni kwamba waabudu makaburi ambao wanawaomba uokozi na msaada maiti wanasema kuwa kuwaomba uokozi huku sio shirki. Wanatumia dalili kisa cha Jibriyl (´alayhis-Salaam) na Ibraahiym (´alayhis-Salaam) pindi alipotupwa ndani ya moto. Imepokelewa ya kwamba Jibriyl alimjia Ibraahiym na kumwambia:

“Je, una haja yoyote?”

Anamuonyesha kuwa anataka kumuokoa. Hapana shaka kuwa Jibriyl (´alayhis-Salaam) ana nguvu kubwa na ana uwezo wa kumuokoa Ibraahiym. Allaah (´Azza wa Jall) amemsifu kwa kusema:

ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ

“Mwenye nguvu kwelikweli na mwenye cheo kwa huyo Mwenye ´Arsh.” (81:20)

Katika Aaya nyingine imekuja:

ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ

“Mwenye muonekano mzuri na nguvu, akalingamana sawasawa.” (53:06)

Bi maana nguvu. Jibriyl akajionyesha kwa Ibraahiym ili aweze kumuokoa kutokamana na janga hili. Ilipokuwa Ibraahiym ni mwenye uaminifu na Allaah (´Azza wa Jall) ndipo akamwambia:

“Kama ni kutoka kwako, hapana. Kama ni kutoka kwa Allaah, ndio.”

Ibraahiym (´alayhis-Salaam) hakutaka kutoka kwa kiumbe amuokoe kutokamana na janga hili. Alimwelekea Mola Wake. Imesihi katika Hadiyth ya kwamba alisema:

حَسْبُنَا اللَّـهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ

“Allaah anatutosheleza. Mzuri alioje mdhamini anayetegemewa!”[1]

Huku ni kwa njia ya kumtegemea Allaah (´Azza wa Jall) na kumwachia mambo yote Yeye. Hii ndio sifa ya viumbe walio na imani kamilifu zaidi kwa vile Ibraahiym alikataa msaada wa kiumbe na akakubali msaada wa Muumba. Kwa kuwa msaada wa kiumbe ndani yake kuna huduma na kumhitajia kiumbe. Kuhusu kupata msaada wa Muumba (Subhaanah) mtu hakupata huduma kutoka kwengine isipokuwa kwa Allaah pekee. Ni fadhila kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Jibriyl alijionyesha kwa Ibraahiym kutaka kumsaidia kitu anachokiweza. Huku ni kutaka msaada kutoka kwa aliye hai na muweza. Hali hii ni kama tajiri kumuonyesha fakiri kutaka kumsaidia pesa. Huku sio kama kuwataka msaada maiti na walioko mbali kama wanavyowataka uokozi waabudu makaburi. Hakika hakuombwi kitu kutoka kwa maiti na wala hawana uwezo juu ya yale wanayoombwa na wala hawasikii wito wa wale wanaowaomba. Amesema (Ta´ala):

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ ۖ لَا يَمْلِكُونَ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَمَا لَهُمْ فِيهِمَا مِن شِرْكٍ وَمَا لَهُ مِنْهُم مِّن ظَهِيرٍ وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ

“Sema: “Waombeni wale mnaodai [kuwa ni waungu] badala ya Allaah, hawamiliki uzito wa chembe ya atomu mbinguni wala ardhini na wala hawana humo ushirika na wala Hana msaidizi miongoni mwao”. Na wala hautofaa uombezi mbele Yake isipokuwa kwa yule Aliyempa idhini.”” (34:22-23)

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ

“Huyo ndiye Allaah, Mola wenu, ufalme ni Wake pekee. Wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende. Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakiyasikia, hawatakuitikieni.” (35:13-14)

[1] 03:173 al-Bukhaariy (05/172).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 115-116
  • Imechapishwa: 12/04/2017