Swali 71: Hivi sasa ummah wa Kiislamu unaishi katika mvurugiko mkubwa, khaswa inapokuja katika dini. Makundi na mapote ya Kiislamu yamekuwa mengi  ambayo yanadai kuwa yanafuata Uislamu sahihi ambao ni lazima kuufuata. Hali imefikia kiasi cha kwamba muislamu anachanganyikiwa hajui amfuate nani na ni nani yuko katika haki.

Jibu: Migawanyiko sio katika dini. Dini imetuamrisha kukusanyika, tuwe kundi moja na ummah mmoja juu ya ´Aqiydah moja na kwamba tumfuate Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ

“Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja Nami ni Mola wenu, basi niabuduni!”[1]

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane!”[2]

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

“Hakika wale waliofarikisha dini yao na wakawa makundi makundi huna lolote kuhusiana na wao. Hakika amri yao iko kwa Allaah, kisha atawajulisha kwa yale waliyokuwa wakifanya.”[3]

Haya ni matahadharisho makali juu ya mifarakano na tofauti. Dini yetu ni dini ya mkusanyiko, urafiki na umoja. Mifarakano sio katika dini. Wingi wa makundi sio katika dini, kwa sababu dini inatuamrisha tuwe kundi moja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Muumini kwa muumini ni kama jengo; upande mmoja unautia nguvu upande mwingine.”[4]

Ni lazima tukusanyike na tuwe kundi moja lililojengeka juu ya Tawhiyd. Mfumo wake uwe ulinganizi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mwenendo wake uwe Uislamu. Amesema (Ta´ala):

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Kwamba hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia za vichochoro nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kumcha.”[5]

Kwa hivyo Uislamu haukubaliani na makundi na mifarakano iliopo hii leo. Bali Uislamu unayakemea kwa ukali na unatuamrisha kukusanyika kwa mujibu wa ´Aqiydah ya Tawhiyd[6].

[1] 21:92

[2] 3:103

[3] 6:159

[4] al-Bukhaariy (2446) na Muslim (2585).

[5] 6:153

[6] Makundi yaliyopo hii leo yanaona kuwa kulingania katika Tawhiyd, kupambana na shirki, kuvunja makuba, kutahadharisha kutokana na Bid´ah na kuwaraddi wanaoenda kinyume na Qur-aan na Sunnah ni sababu zinazopelekea katika mifarakano na hazikusanyi. Hawajui kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitumilizwa katika wakati ambapo watu na magomvi kati yao ambapo baadaye Allaah akawakusanya kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Tawhiyd. Wako wapi wabusara na na wenye akili? Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeye mwenyewe amekuja kufarikisha kati ya watu. Malaia walisema:

”Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amegawanya kati ya watu.” (al-Bukhaariy (6852))

Amegawanya kati ya muumini na kafiri, haki na batili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 177-179
  • Imechapishwa: 04/07/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy