71. Qur-aan na Sunnah vinatakiwa kuhukumu akili, na si kinyume chake

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

57 – Hadiyth zote Swahiyh zilizopokelewa kuhusu hilo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mambo ni kama alivosema.

58 – Maana yake ni kama alivokusudia.

59 – Hatutoingilia kupekua jambo hilo hali ya kupindisha maana kwa maoni yetu wala kufikiria kwa matamanio yetu.

MAELEZO

Kila kilichopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu kuthibitisha Kuonekana ni haki na ni kweli. Ni kama mfano wa yaliyotajwa ndani ya Qur-aan. Ni lazima kuyaamini kwa sababu maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Wahy kutoka kwa Allaah:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

”Hatamki kwa matamanio yake. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.”[1]

Sunnah ni Wahy wa pili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza katika Hadiyth nyingi na zilizopokelewa kwa mapokezi mengi ya kwamba waumini watamuona Mola wao siku ya Qiyaamah. Kwa hivyo ni lazima kuamini jambo hilo pasi na kulifanyia namna wala kulipotosha, kulipigia mfano wala namna. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maana yake ni kama alivokusudia.”

Alivyokusudia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), si kama walivyokusudia wazushi na wapotoshaji. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hatutoingilia kupekua jambo hilo hali ya kupindisha maana kwa maoni yetu wala kufikiria kwa matamanio yetu.”

Kama wanavyofanya Jahmiyyah, Mu´tazilah na wanafunzi wao na wakachukua maoni yao batili ya kupindisha maana. Ni lazima kwetu kufuata Qur-aan na Sunnah na wala tusiingize akili na fikira zetu na tukazifanya kuhukumu Qur-aan na Sunnah. Ni lazima kuifanya Qur-aan na Sunnah vikahukumu akili na fikira.

[1] 53:3-4

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 80-81
  • Imechapishwa: 18/01/2023