Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

60 – Hakuna aliyesalimika katika dini yake isipokuwa yule aliyejisalimisha kwa Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akarudisha elimu ya yale yanayomtatiza kwa yule mwenye kuyajua.

MAELEZO

Bi maana akakubali yale yote yaliyokuja kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akayaamini kama yalivyokuja pasi na kuyakengeusha wala kuyapindisha maana. Hii ndio maana ya kujisalimisha. Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Nimemuamini Allaah na yaliyokuja kutoka kwa Allaah kama alivyokusudia Allaah. Vilevile nimemuamini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yaliyokuja kutoka kwa Mtume wa Allaah kama alivyokusudia Mtume wa Allaah.”[1]

Na si kutokana na matamanio, upotoshaji na maoni ya watu.

Yule mwenye kuamini, akasajilimisha na akarudisha yale yanayomtatiza kwa sababu ya kutojua maana yake, ikiwa ameshindwa kujua maana yake basi hatojua hata namna yake, anatakiwa kurudisha kwa mtambuzi wake ambaye ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Yule ambaye anatatizika na kitu basi anatakiwa kurejea kwa wanazuoni. Ikiwa wanazuoni pia hawajui jambo hilo, basi ni lazima kuegemeza jambo hilo kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa).

[1] Tazama ”al-Fataawaa al-Hamawiyyah al-Kubraa”, uk. 121 ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 81-82
  • Imechapishwa: 18/01/2023