Makadirio yana upambanuzi. Kuna makadirio yaliyotangulia na makadirio yaliyopambanuliwa.

Miongoni mwa makadirio yaliyopambanuliwa ni pamoja na kipomoko tumboni mwa mama yake, makadirio yanayokuwa kwenye usiku wenye cheo, makadirio yaliyotokea pindi alipoumbwa Aadam na Allaah akagusa kizazi chake kwenye mgongo wake. Haya ni makadirio ya upambanuzi. Makadirio ya muda wa kueshi, makadirio ya kila mwaka katika usiku wenye cheo na makadirio ya kila siku yote ni upambanuzi wa makadirio yaliyotangulia na yanarejea katika yale makadirio yaliyotangulia. Kipomoko wala kiumbe kingine hakina namna ya kujitoa katika yaliyoandikwa kwenye makadirio yaliyotangulia. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa yamekwishaandikwa makazi yake Peponi na makazi yake Motoni.” Wakasema: ”Ee Mtume wa Allaah! “Si tutegemee basi tuliyoandikiwa na tuache kutenda?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Fanyeni matendo! Kwani hakika kila mmoja ni mwenye kufanyiwa wepesi juu ya kile alichoumbiwa. Kuhusu ambaye ni katika wenye furaha, atafanyiwa wepesi wa kufanya matendo ya wenye furaha. Kuhusu ambaye ni katika wala khasara atafanyiwa wepesi wa kufanya matendo ya wala khasara.” Kisha akasoma maneno Yake (Ta´ala):

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ

“Basi yule anayetoa na akamcha Allaah na akasadikisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi. Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza na akakadhibisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu.”[1]

Huu ni utafiti mkubwa ambao unatakiwa kuhifadhiwa na kudhibitiwa. Kwa ´Aqiydah hii mtu anajipambanua na mapote yote ya Bid´ah na upotevu, kama vile Qadariyyah wakanushaji na Jabriyyah. Wote utakuwa ni mwenye kwenda kinyume nao na wewe utakuwa ni mwenye kuitakidi I´tiqaad ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

[1] 92:05-10 al-Bukhaariy (4949) na Muslim (2647).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 104-105
  • Imechapishwa: 03/11/2024