71. Allaah anatakiwa kushukuriwa kwa hali yoyote ile

Kuridhia ni katika matendo ya moyo na ukamilifu wake ni sehemu ya kushukuru. Kuna hata wanachuoni waliofasiri kuridhia kama kushukuru. Kwa ajili hii ndio maana Allaah anahimidiwa katika Qur-aan na Sunnah kwa hali yoyote ile. Katika hiyo kunaingia kuridhia hukumu ya Allaah. Imekuja katika Hadiyth:

“Wa kwanza ambao wataitwa kuelekea Peponi ni wale wenye kumhimidi Allaah katika kipindi cha raha na kipindi kizito.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipokuwa akiona kitu cha kumfurahisha anasema: “Himdi zote ni za Allaah ambaye kwa neema Zake yanatimia mambo mema.” Pindi anapoona kitu kisichomfurahisha husema: “Himdi zote ni za Allaah kwa hali yoyote.”

Imeshatangulia ya kwamba Imaam Ahmad amepokea katika “al-Musnad” yake kupitia kwa Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) husema: “Ee Malaika wa mauti! Umemchukua mtoto wa mja wangu? Umechukua kipumbazo cha macho yake na matunda ya moyo wake?” Ndipo atajibu: “Ndio.” Allaah aseme: “Alisema nini?” Ajibu: “Amekushukuru na kusema “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” Ndipo Allaah aseme: “Mjengee mja Wangu nyumba Peponi na ipeni jina “Nyumba ya shukurani”.”

Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye ambaye atabeba bendera ya Himdi. Ummah wake ndio wenye kumhimidi Allaah sana katika nyakati za raha na za shida. Shukurani juu ya ridhaa kuna uhusiano aina mbili:

1- Mja anatambua kuwa Allaah (Subhaanah) ana haki ya hilo, amekiumba kila kitu kwa njia nzuri kabisa na amekiimairi kila kitu na kwamba Yeye ni mjuzi na Mwenye hekima wa yote.

2- Mja anatambua kuwa kile Allaah alichomchagulia mja Wake muumini ni bora kuliko kile mja alichojichagulia Mwenyewe. Muslim amepokea kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninaapa kwa ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake kwamba Allaah hampangii kitu mja Wake muumini isipokuwa inakuwa ni kheri kwake na hilo haliwi isipokuwa kwa muumini. Anapofikwa na kitu kizuri, anashukuru na inakuwa ni kheri kwake. Anapofikwa na dhara, anasubiri na inakuwa ni kheri kwake.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa kila kile ambacho Allaah anampangia mja Wake muumini ni kheri kwake iwapo atasubiri juu ya majaribio na kumshukuru juu ya neema. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ

“Hakika katika hayo kuna alama kwa kila mwingi wa ustahamilivu na wa kumshukuru [Allaah].” 31:31

Hata hivyo mipango ya Allaah haipelekei kuwa ni kheri kwa ambaye hasubiri juu ya majanga wala kushukuru kipindi cha raha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 158-159
  • Imechapishwa: 09/11/2016