70. Ukafiri wa anayedai kuwa ni Mtume na ukafiri wa anayemsadikisha

Maneno yake:

“… ndiye mwisho wa mwisho Manabii na Mitume.”

Yeye ndiye Mtume wa mwisho. Hakuna baada yake isipokuwa kusimama kwa Qiyaamah. Kwa ajili hiyo anaitwa “Mtume wa Saa”. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimetumilizwa mimi na Saa namna hii”; akaashiria kidole cha shahada na kidole cha katikati.”[1]

Yeye ni Mtume wa Saa. Kutumilizwa kwake ni miongoni mwa alama za Qiyaamah. Hakuna Mtume mwingine baada yake. Amesema (Ta´ala):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.”[2]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika watakuwa baada yangu waongo thelathini; kila mmoja katika wao atadai kuwa ni Nabii ilihali mimi ndiye mwisho wa Manabii – hakuna Nabii mwingine baada yangu.”

Ambaye haamini kuwa ujumbe umekhitimishwa naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kafiri. Kwa msemo mwingine ambaye anaona kuwa inafaa akatumilizwa Nabii mwingine baada ya Mtume ni kafiri. Kwa sababu atakuwa ni mwenye kumkadhibisha Allaah, Mtume Wake na maafikiano ya waislamu. Kwa mfano Qaadiyyaaniyyah ambao wanaamini unabii wa Ghulaam al-Qaadiyaaniy. Vivyo hivyo wale wenye kuamini unabii wa Musaylamah na unabii wa al-Aswad al-´Ansiy.

Ambaye anadai unabii baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kitendo hicho ni chenye kumfanya kuritadi nje ya Uislamu. Akitubia basi Allaah anamsamehe. Kwa mfano wa Twalhah al-Asadiy ambaye alidai kuwa ni Nabii kisha akatubia juu ya hilo ambapo Allaah akamsamehe na akauliwa hali ya kuwa ni shahidi (Radhiya Allaahu ´anh). Sajaah at-Tamiymiyyah ambaye alidai kisha akatubia ambapo Allaah akamsamehe. Kuhusu mwenye kudai kuwa ni Mtume au akamsadikisha mwenye kudai hivo ni kafiri na ni mwenye kuritadi nje ya dini ya Uislamu. Kwa kuwa hakuna Nabii mwingine baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wala hakuna haja ya Nabii baada ya Mtume na wala hakuna haja ya kuteremshwa Kitabu kingine baada ya Qur-aan. Kwa sababu Allaah amewatosheleza walimwengu kwa Mtume huyu na kwa Kitabu hiki. Ujumbe wake ni wenye kuenea katika kila wakati na mahali. Ni wenye kuenea katika wakati mpaka Qiyaamah kisimame. Na ni wenye kuenea katika mahali dunia nzima. Yote ni yenye kuenea mpaka Qiyaamah kisimame na ni yenye kuwatosheleza viumbe wote. Mitume hutumwa wakati kuna haja. Walimwengu hawana haja ya kutumilizwa Mtume au kuteremshwa Kitabu baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na baada ya Qur-aan.

[1] al-Bukhaariy (6503, 6504) na Muslim (2950, 2951) kupitia kwa Sahl bin Sa´d na Anas (Radhiya Allaahu ´anhum).

[2] 33:40

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 100-101
  • Imechapishwa: 18/05/2021