3 – Miongoni mwa sababu za kuhifadhi tupu ni kumkataza mwanamke kusafiri peke yake bila Mahram wa kumlinda na kumuhifadhi kutokamana na tamaa za wachezaji na wachafu. Imekuja katika Hadiyth Swahiyh zinazomkataza mwanamke kusafiri pasi na Mahram. Moja wapo ni ile iliopokelewa na Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asisafiri mwanamke siku tatu isipokuwa awe pamoja naye Mahram.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Abu Sa´iyd (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Amekataza mwanamke kusafiri mwendo wa siku mbili au nyusiku mbili isipokuwa awe pamoja naye mume wake au Mahram.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si halali kwa mwanamke kusafiri mwendo wa mchana mmoja na usiku isipokuwa awe pamoja naye na Mahram.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Makadirio katika Hadiyth ya siku mbili, siku tatu, mchana mmoja na usiku wake, makusudio ni zile safari zilizokuwa kwa njia ya vyombo vya kusafiria zilizokuwa zinajulikana wakati huo katika kusafiri na miguu na wanyama. Kutofautiana kwa Hadiyth katika makadirio haya kwa siku tatu, siku mbili, mchana mmoja na usiku wake na zilizo chini ya hapo, wanachuoni wamejibu kwamba makusudio sio udhahiri wake na kwamba makusudio ni zile zote zinazoitwa kuwa ni safiri kwamba mwanamke amekatazwa nazo. Imaam an-Nawawiy amesema katika “Sharh Swahiyh Muslim”:

“Kwa ufupi ni kwamba zile zote zinazoitwa ´safari` mwanamke amekatazwa pasi na kuwa na mume au Mahram. Ni mamoja ikawa siku tatu, siku mbili, siku moja, kilomita moja au vyenginevyo. Hayo ni kutokana na upokezi wa Ibn ´Abbaas uliosema kwa kuachilia; ndio upokezi wa mwisho wa Muslim uliotangulia:

“Asisafiri mwanamke isipokuwa awe pamoja na Mahram.”

Hii imekusanya zile zote zinazoitwa ´safari`. Allaah ndiye mjuzi zaidi.”[1]

Kuhusu wale waliomtolea fatwa mwanamke kufaa kusafiri pamoja na kundi la wanawake kwenda hajj ambayo ni ya wajibu ni jambo linalokwenda kinyume na Sunnah. Imaam al-Khattwaabiy amesema katika “Ma´aalim-us-Sunnah”:

“Pamoja na Tahdhiyb ya Ibn-ul-Qayyim: “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemzuia mwanamke kusafiri isipokuwa awe pamoja na mwanamume ambaye ni Mahram yake. Kwa hiyo kumhalalishia kusafiri kwenda hajj pamoja na kutopatikana sharti iliyothibitishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jambo linalopingana na Sunnah. Ikiwa kutoka kwake bila Mahram ni maasi basi haitojuzu kumlazimishia hajj. Ni kutii amri inayopelekea katika maasi.”[2]

Hawakumhalalishia mwanamke kusafiri moja kwa moja bila Mahram. Wamemhalalishia hilo kusafiri kwenda katika safari ya hajj ilio ya wajibu peke yake. Imaam an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´” amesema:

“Haijuzu katika safari za sunnah, safari za biashara, za matembezi na mfano wazo isipokuwa awe pamoja na Mahram.”[3]

Wale ambao wanachukulia wepesi katika zama hizi kumwacha mwanamke akasafiri bila Mahram katika safari zote hakuna mwanachuoni yeyote katika wale ambao zinategemewa kauli zao anayekubaliana nao. Maneno yao kwamba Mahram amsindikize na kumpandisha ndani ya ndege kisha apokelewe na Mahram yake mwingine wakati atapofika katika nchi anayokwenda – kwa sababu wanadai kuwa eti ndege ni yenye kuaminika kwa kuwa ina wasafiri wengi waume kwa wake – tunawaambia hapana; ndege ina khatari zaidi kuliko kipando kingine. Kwa sababu wasafiri huchanganyika ndani yake na pengine mwanamume akakaa kando ya mwanamke, pengine ndege ikafikwa na sababu itayopelekea ikageuza kwenda kudema uwanja mwingine na hivyo asimpate wa kumpokea. Matokeo yake anakuwa ni mwenye kujiweka khatarini. Mwanamke anakuwa katika hali gani katika nchi ambayo haijui na wala hana Mahram ndani yake!

[1] (09/103).

[2] (02/276-277).

[3] (08/249).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 122-124
  • Imechapishwa: 11/12/2019