70. Kulia baada ya kufiliwa na mtoto na kuwa radhi na makadirio ya Allaah

Kumetangulia kutajwa aliyosunisha na kuyakataza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa wenye msiba. Miongoni vilevile mwa mambo aliyoyasunisha ni kuwa na unyenyekevu, kulia pasi na kutoa sauti na kuwa na moyo wa huzuni. Alifanya hivo na kusema:

“Hakika macho hutokwa na machozi na moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu.”

Kadhalika imesuniwa kumshukuru Allaah na kusema:

“Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

Miongoni mwa Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuwa radhi na Allaah wakati wa msiba na nyakati zengine. Hayapingani na kububujikwa na machozi na kuwa na moyo wenye huzuni. Hakuna watu waliokuwa na bidii kwelikweli ya kumridhisha Mola wao kama Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Ibn Abiyd-Dunyaa amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika sisi Mitume hupewa majaribio mara mbili.”

Ndio maana Mtume na mja aliyekuwa ni mwenye kuridhiwa sana na mipango na makadirio ya Allaah ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuna mja anayemhimidi Allaah zaidi kama yeye. Pamoja na hivyo alilia pindi mvulana wake Ibraahiym alipokufa. Alilia kwa sababu ya rehema, huruma na hisia kwa mwanaye na wakati huohuo moyo wake ulikuwa ni wenye kumridhia na kumshukuru Allaah na ulimi wake ulikuwa ni wenye kushughulika na kumhimidi na kumdhukuru.

Kwa kuzingatia mambo haya mawili makubwa – huruma kwa mtoto aliyekufa na kuridhia mipango ya Allaah – kunaweza kuwa uzito kuyakusanya, kuna wanachuoni kutoka katika Salaf waliocheka pindi watoto wao walipofariki. Walipoulizwa ni vipi wanaweza kucheka katika hali kama hii, wakasema:

“Allaah amepanga hukumu Yake na nimependa kuwa radhi na hukumu Yake.”

Hili liliwatatiza wanachuoni wengi na wale vigogo wa Taswawwuf. Ni vipi ataweza kulia Mtume wa Mola wa walimwengu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku aliyofariki mtoto wake, ilihali yeye ndiye kiumbe mwenye kuridhiwa zaidi na Allaah, na mwanachuoni huyu akafikia radhi kama hii mpaka akacheka kwa ajili ya mwanaye? Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Uongofu wa Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mkamilifu zaidi kuliko uongofu wa mwanachuoni huyu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliipa ´ibaadah haki yake. Kwa ajili hiyo moyo wake ulikuwa unaweza kupata nafasi ya kuwa radhi na Allaah na kuwa na huruma kwa mtoto. Akamhimidi Allaah na kuridhia mipango Yake. Alilia kwa sababu ya huruma na hisia. Huruma wake ndio uliyomfanya kulia na ´ibaadah na mapenzi yake kwa Allaah ndio vilivyomfanya kumridhia na kumshukuru Allaah. Moyo wa mwanachuoni huyu haukupata nafasi wa vyote viwili. Kwa ajili hiyo ´ibaadah ya kuwa radhi ikamshughulisha kutokamana na ´ibaadah ya huruma na hisia – na Allaah (Ta´ala) ndiye anajua zaidi.”

Yanayozidi kutilia nguvu haya aliyosema Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) ni kisa cha Ya´quub (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alijawa na machozi kisha akasema:

فَصَبْرٌ جَمِيلٌ

“Subira ni njema… ” 12:83

إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Hakika mimi machozi na huzuni wangu namshitakia Allaah na najua kutoka kwa Allaah kitu msichokijua.” 12:86

Alihisi hisia na huruma pindi:

وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ

“Macho yake yakageuka meupe [kwa kulia] kutokana na huzuni.” (12:84)

Mfumo wa Ya´quub (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni bora kuliko mfumo wa mwanachuoni huyu. Pamoja na kuwa Ya´quub alikuwa na watoto wengi lakini akaonyesha huruma na hisia kama hii ilihali mwanachuoni huyu hakuwa na zaidi ya mtoto aliyekufa. Thaabit al-Bunaaniy amesema:

“Silah bin Ushaym alikuwa vitani pamoja na mtoto wake. Akamwambia: “Mwanangu kipenzi! Sogea mbele upigane mpaka uuawe ili niweze kutarajia malipo kutoka kwa Allaah kwa sababu ya subira nitayofanya. Akasogea mbele akapigana mpaka akauawa. Baada ya hapo baba yake na yeye akasogea mbele akapigana mpaka akauawa. Wanawake walipokusanyika mke wake Mu´aadhah al-´Adhriyyah akawaambia: “Ikiwa mmekuja kwa ajili ya kunipa hongera karibuni. Ikiwa mmekuja kwa sababu nyingine rejeeni.”

Ibn-ul-Jawziy ameeleza kuwa Abu Juhayfah amesema:

“Tulikuwa njiani tukielekea Hamadhaan na tulikuwa na mwanaume kutoka ´Azd. Tahamaki akaanza kulia. Nikamwambia: “Unahuzunika?” Akasema: “Hapana, lakini nimemuacha mwanangu nyumbani na nimetamani lau ningekuwa naye tukaingia Peponi sote pamoja.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 156-158
  • Imechapishwa: 09/11/2016