7. Suufiyyuun wanavowatakasa Mashaykh zao

Ndugu watukufu! Haya ndio madhehebu ya Suufiyyah. Ambayo ni mepesi kidogo ni yale yalio na utawa – jambo ambalo limekatazwa katika Uislamu – wakati machafu zaidi ni yale yanayosema kwamba Allaah amekita ndani ya viumbe Wake na kwamba kila kitu ni Allaah. Isitoshe mapote yote ya Suufiyyah ni yenye kupetuka mipaka katika kuwatakasa Mashaykh na mwanafunzi ni mwenye kuwa na unyenyekevu kikamilifu mbele ya Shaykh wake, kiasi cha kwamba mwanafunzi anakuwa ni mwenye kumtii Shaykh utiifu wa kikamilifu na usiokuwa na kipingamizi chochote. Hali inafikia mpaka mwanafunzi mbele ya Shaykh anakuwa kama mfano wa maiti mikononi mwa mwoshaji.

Muhammad ´Uthmnaan as-Suufiy – mwandishi wa “al-Habaat al-Muqtabisah” – amesema wakati alipokuwa anazungumzia adabu za mwanafunzi anayetakiwa:

“Miongoni mwazo anatakiwa kukaa mbele yake kama jinsi anavyokaa wakati anaposwali, kuanguka mbele yake na asikae juu ya mkeka wake, asitawadhe kwenye birika lake na asishegame kwenye fimbo yake. Sikiliza waliyosema watu watukufu: “Mwenye kusema kumwambia Shaykh wake, kwa nini?, hatofaulu kamwe”.”

Mustwafaa al-Bakriy ameandika sifa hizi kwenye shairi lake Bulghat-ul-Muriyd na kusema:

“Lisalimishe jambo lako lote kwake na usiwe na upinzani, hata kama atakuja na kitu cha dhambi. Kuwa mbele yake kama maiti, kwa kuwa niko na yule anayeniosha ili anioshe uchafu wangu. Usikanyage kwa mguu yako juu ya mkeka wake na usilale juu ya mto wake.”[1]

Suufiyyuun wamemfaradhishia mwanafunzi kuwa mtumwa wa kifikra na wa kimwili mbele ya Shaykh na kama mfano wa maiti inayooshwa isiyokuwa na utashi wowote. Lau hata atamuona anafanya maasi au anaenda kinyume na Shari´ah, bado itakuwa haijuzu kwake kumuuliza kwa sababu gani. Lau atafanya hivo, ataondoshewa rahmah za Shaykh wake na hivyo hatofaulu kamwe. Hii ni miongoni mwa sababu ya kupotea kulikokuwa kukubwa kwa Suufiyyuun. Wamejiondoshea kukataza maovu, kwa kiasi cha kwamba wakawa wanaonelea maovu kuwa ni mema, bali kujikurubisha kwa Allaah na karama. Ama kuhusu mafunzo sahihi ya Uislamu ni kwamba haijuzu kumtii yeyote katika kitu cha maasi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haijuzu kumtii kiumbe yeyote katika kumuasi Muumba.”[2]

Hili linahusiana hata na wazazi wawili ambao wana haki zaidi kuliko mwengine yeyote. Haijuzu kuwatii katika kumuasi Allaah. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖوَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا

“Lakini wakikung´ang´ania kwamba unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii na tangamana nao kwa wema duniani.” (Luqmaan 31:15)

[1] al-Wakiyl katika “Bughat-ul-Muriyd.

[2] Swahiyh. Ameipokea Ahmad. Tazama “as-Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swaghiyr”.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqiyqat-us-Suufiyyah
  • Imechapishwa: 24/12/2019