07. Ni lazima kwetu kujizuia na daku pale adhaana inapoanza kutolewa?

Swali 07: Ni lazima kwetu kujizuia na daku pale adhaana inapoanza kutolewa au inafaa kwetu kula na kunywa mpaka muadhini amalize kuadhini?

Jibu: Ikiwa muadhini anatambulika kuwa haadhini isipokuwa mpaka kupambazuke basi ni lazima kujizuia na kula na kunywa na mambo mengine yote yenye kufunguza pale kunapoanza kuadhiniwa. Ama ikiwa adhaana zinatolewa kwa kudhania na kuchunga lililo salama zaidi (الإمساك) kwa mujibu wa jadwali[1], basi hakuna neno kunywa na kula wakati kunapoadhiniwa. Hayo yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Bilaal anaadhini usiku. Hivyo kuleni na kunyweni mpaka aadhini Ibn Umm Maktuum.”

Mpokezi amesema katika Hadiyth nyingine:

“Ibn Umm Maktuum alikuwa haadhini mpaka aambiwe: kumekucha. Kwa kuwa alikuwa ni mtu kipofu. Kwa hivyo alikuwa haadhini mpaka aambiwe kuwa kumekuja. Bi maana asubuhi imeanza.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/04-hadiyth-tulikula-daku-pamoja-na-mtume-wa-allaah-swalla-allaahu-alayhi-wa-sallam/

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdllaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah tata´alaqah bisw-Swiyaam, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 11/04/2019