7. Nafasi na uhusiano wa Sunnah kwa Qur-aan

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sunnah kwetu ni mapokezi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sunnah inaifasiri na kuiweka wazi Qur-aan.”

Amesema “Sunnah kwetu ni mapokezi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Sunnah ni nini? Ni mapokezi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bi maana maneno yake, matendo yake na yale aliyoyakubali. Tuna Qur-aan na Sunnah. Sunnah ni mapokezi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); maneno yake, matendo yake na yale aliyoyakubali. Hayo ndio ambayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ametufaradhishia kuyafuata na kushikamana nayo. Amesema wakati alipokuwa akibainisha nafasi ya Sunnah na mafungamano yake na Qur-aan:

“Sunnah inaifasiri na kuiweka wazi Qur-aan.”

Sunnah inaibainisha Qur-aan:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao.”[1]

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ

“Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume.”[2]

Kurejea kwa Allaah inahusiana na kurudi katika Qur-aan na kurejea kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inahusiana na kurudi kwake wakati wa uhai wake na katika Sunnah zake baada ya kufa kwake; yako katika ngazi moja. Kama mfano wa Qur-aan Sunnah nayo inatumiwa kama dalili na marejeo katika mambo ya ´Aqiydah, hukumu, ya halali na ya haramu na mambo mengine yote ya dini. Kwa ajili hiyo Salaf walipokuwa wanapata maswali yanayohusiana na ´Aqiydah au mambo mengine wanajibu kwa ile dalili wanayoanza kuiangukia katika Qur-aan au Sunnah. Hawakuwa wakitofautisha kati ya Qur-aan na Sunnah. Tutataja mfano wa hilo na jinsi ulivyokuwa msimamo wa ´Umar, Abu Bakr, Ibn ´Umar na Maswahabah wengine.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na kuiweka wazi Qur-aan.”

Sunnah inabainisha na kupambanua yale mambo ya jumla katika Qur-aan, kuyaweka wazi mambo yasiyokuwa wazi, kuyafungamanisha mambo ambayo hayakufungamanishwa, kuyafanya maalum mambo ambayo yako kwa jumla. Sunnah inatuwekea wazi swalah, nyakati zake, idadi zake, upambanuzi wake, kipi tunachotakiwa kusoma ndani yake, kipi tunachotakiwa kusema katika Rukuu´, kipi tunachotakiwa kusema katika Sujuud. Yote haya yanapatikana katika Sunanh. Mara nyingi Allaah anasema:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ

“Simamisheni swalah.”[3]

Inawekwa wazi na kupambanuliwa na Sunnah. Sunnah inafafanua, inabainisha na kuweka wazi mambo ambayo yako kwa jumla katika Qur-aan, inayafanya kuwa maalum mambo ya kijumla na kuyafungamanisha mambo ambayo hayakufungamanishwa. Ni kama alivyosema Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah):

“Sunnah inaifasiri na kuiweka wazi Qur-aan.”

[1] 16:44

[2] 04:59

[3] 02:43

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 369-370
  • Imechapishwa: 23/07/2017