Karne zilizotangulia na zilizokuja nyuma zimezungumza kwa kina juu ya kuridhia, wakalipambanua suala hilo na kulitilia umuhimu. Hii ni dalili inayoonyesha ujuu wa ngazi yake. ´Amr bin Aslam amesimulia kuwa amemsikia Abu Mu´aawiyah al-Aswad akisema kuhusu maneno ya Allaah (Ta´ala):

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً

“Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake ilihali ni muumini, Tutamhuisha maisha mazuri.” 16:97

“Bi maana kuridhia na kukinai.”

Maalik bin Anas amesema:

“Nilifikiwa na khabari kwamba Abud-Dardaa´ aliingia kwa mtu alikuwa katika kukata roho na huku anamshukuru Allaah. Abud-Dardaa´ akasema: “Umefanya vizuri. Allaah (Ta´ala) anapenda mipango Yake kuipokea kwa kuridhia.”

Ibn Abiy Dunyaa amepokea kwa mlolongo wa wapokezi wake kupitia kwa Ibn ´Awn aliyesema:

“Ridhia mipango ya Allaah sawa ikiwa ina uzito na wepesi. Hakika hilo linakufanya kuwa na wasiwasi kidogo na angalia lengo lako zaidi iwe ni Aakhirah. Tambua kuwa mja hafikii uhakika wa kuridhia mpaka kuridhia kwake wakati wa ufukara na majanga iwe ni kama kuridhia kwake wakati wa utajiri na raha. Vipi utamuomba Allaah akuhukumu kisha unakasirika pindi unapoona kuwa mipango Yake inaenda kinyume na matamanio yako? Pengine kuangamia kwako kuko katika hayo unayotamani. Vipi unaweza kumuomba Allaah akuhukumu kisha unaridhia pale unapoona kuwa mipango Yake inaendana na matamanio yako? Hilo linatokamana na uchache wa elimu yako kuhusu mambo yaliyofichikana. Vipi unaweza kumuomba Allaah akuhukumu ikiwa uko namna hiyo? Hukuwa ni mwenye inswafu juu ya nafsi yako na wala hukuridhia.”

Hafsw bin Humayd amesema:

“Nilikuwa kwa ´Abdullaah bin al-Mubaarak Kuufah pindi mke wake alipokufa. Nikamuuliza maana ya kuridhia. Akajibu: “Kuridhia ni kutotamani kuwa na hali nyingine.” Halafu akaja Abu Bakr bin ´Ayyaash kutoa pole juu ya msiba. Mimi sikumjua. ´Abdullaah akasema: “Muulize yale tuliokuwa tukizungumza.” Nikamuuliza akasema: “Mwenye kuzungumza kwa njia yenye kuashiria kuridhia ameridhia.” Nikamuuliza al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw juu ya hilo akasema: “Hivyo ndivyo wanakuwa wasomi.” ad-Daylamiy alimuuliza al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw: “Ni nani mwenye kuridhia?” Akasema: “Ni yule asiyetaka kuwa katika hali nyingine kuliko ile ambayo tayari yukoemo.”

Sayyaar amesema:

“Nilimtembelea Abul-´Aaliyah alipokuwa katika kukata roho. Akasema: “Ninapenda zaidi kile kinachopendwa zaidi na Allaah.”

Sufyaan ath-Thawriy amesema:

“´Umar bin ´Abdil-´Aziyz alisema kumwambia mwanaye: “Unasikia vipi?” Akasema: “Nasikia mauti.” Akasema: “Napenda zaidi wewe uwe katika mizani yangu kuliko mimi kuwa katika mizani yako.” Mtoto akamwambia: “Ninaapa kwa Allaah babangu kipenzi! Napenda zaidi yatimie yale unayotamani kuliko yatimie yale ninayotamani.”

Imaam Ahmad amepokea katika “az-Zuhd” kupitia kwa ´Aliy bin Abiy Twaalib aliyesema pindi Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alipokufa:

“Tumeridhia mipango ya Allaah na tumejisalimisha na amri Yake. Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 154-156
  • Imechapishwa: 07/11/2016