69. Mwenye busara na msimamo wake wa dunia

1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayepambaukiwa katika nyinyi hali ya kuwa ni mwenye amani katika familia yake, mzima kwenye kiwiliwili chake na tonge la siku yake, basi ni kana kwamba amekusanyiwa yeye dunia kwa pembe zake zote.”

2 – Ni wajibu kwa mwenye busara asighurike na maisha ya dunia hii na mapambo yake ili isije kumshughulisha kutokamana na Aakhirah ambayo ndio itakayodumu milele. Ayazingatie maisha haya kama Allaah alivyoyazingatia. Inapelekea katika matokeo yasiyokuwa na mwisho. Majengo yake yataharibika na wakazi wake watakufa. Mapambo yake yataondoka na kijani chake kitatokomea.

3 –  Hakuna kiongozi mkandamizi na mwenye kuamriwa wala fakiri masikini anayedharauliwa isipokuwa atakunywa katika kikombe cha kifo. Baada ya hapo watabebwa ndani ya udongo na kuoza mpaka wapotee. Baadaye atairithi ardhi na vyote vilivyomo ndani yake Yule ambaye ni mtambuzi wa yaliyofichikana.

4 – Mwenye busara hatakiwi kuitegemea dunia ambayo iko namna hii. Asijihisi utulivu juu ya dunia ambayo iko kwa sifa hii. Yanamsubiri yale ambayo kamwe hakuna macho yamekwishayaona, sikio limekwishayasikia wala yamekwishampitikia mtu moyoni.

5 – Dunia ni bahari iliyojaa. Watu wanaogolea juu ya mawimbi yake. Masiku ni yenye kupigwa mfano juu ya watu. Kila kinachoelekea kutokomea kimefanana na wao. Yule mwenye kupewa mambo matatu katika dunia hii basi amekusanyiwa dunia nzima; amani, riziki na uzima. Hakuna mwingine anayeghuriwa na kitu katika dunia isipokuwa mdanganyifu tu.

6 – Mwenye busara anatambua kwamba yale ambayo hayakubaki kwa wengine basi kwake pia hayatobaki. Anatambua kwamba yale ambayo yamepokonywa kutoka kwa wengine hatoachiwa yeye.

7 – Yule ambaye anataka kuwa huru basi ajiepushe na mambo ya matamanio ijapo ni yenye kupendeza. Si kila chenye kupendeza kinanufaisha, lakini kila chenye kunufaisha ni chenye kupendeza. Matamanio yote ni yenye kuchosha baada ya muda fulani. Isipokuwa tu faida na faida kubwa ni Pepo na mtu asimuhitajie mwingine zaidi ya Allaah.

8 – Ma´n bin ´Awn amesema:

“Ni wangapi wanaoianza siku na hawaikamilishi?  Ni wangapi wanaoisubiri kesho na hawaifiki? Kama mtaangalia malipo na njia ya kuyaendea basi mngelichukia mipango ya baadaye.

9 – Sababu inayomfanya mwenye akili kuyazingatia maisha haya ya dunia ipasavyo ni yeye kutoitegemea na badala yake atangulize yale ayawezayo ili aweze kupata maisha yenye kudumu na neema za milele. Aidha aache mipango mirefu ya baadaye. Afikiri kuwa anaweza kufariki wakati wowote.

10 – Mwenye busara anatakiwa kuacha mipango mirefu ya baadaye. Badala yake anatakiwa kuzingatia wale watu waliotangulia hapo kabla. Athari zao zimepotea. Khabari zao zimekatika. Hakuna kilichobaki kwao isipokuwa utajo peke yake. Hakuna chochote kilichobaki katika majumba yao isipokuwa michoro peke yake. Ametakasika kutokamana na mapungufu Yule ambaye ni muweza wa kuwahuisha na kuwakusanya kwa ajili ya kuwalipa na kuwaadhibu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 277-281
  • Imechapishwa: 09/09/2021