69. Allaah hahitaji ´Arshi – ´Arshi ndio inamuhitaji Allaah

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ

“Naye hapingiki Aliye Mkuu kabisa juu ya waja Wake.”[1]

Amejisifu Mwenyewe ya kuwa yuko juu ya viumbe Wake. Maana yake ni ujuu wa dhati. Allaah kwa dhati Yake (Subhaanah) yuko juu ya viumbe Wake. Hakuna chochote katika viumbe Wake kilichopo ndani ya dhati Yake wala ndani ya dhati Yake hakuna chochote katika viumbe Wake. Kwa ajili hiyo Salaf wakasema kuwa Allaah ametengana na viumbe Wake. Kwa maana nyingine mbalimbali na ametengana navyo. Hapa wanaraddiwa Huluuliyyah ambao wanadai kuwa Allaah yuko kila mahali  – Allaah ametakasika kutokana na yale wanayoyasema!

´Arshi ndio paa la viumbe na ndio kiumbe kilicho juu zaidi na kikubwa zaidi. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu ya ´Arshi kwa njia inayolingana na utukufu Wake. Si kama ujuu wa kiumbe juu ya kiumbe kingine. Kwa msemo mwingine hakusemwi kuwa anaihitaji ´Arshi. Allaah yuko juu ya ´Arshi lakini si Mwenye kuihitaji – bali ´Arshi ndio yenye kumuhitaji Allaah (´Azza wa Jall):

إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا ۚ وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ

“Hakika Allaah anazuia mbingu na ardhi zisiondoke na zikiondoka basi hakuna yeyote wa kuzishikilia baada Yake.”[2]

Mbingu, ardhi, ´Arshi na viumbe wengine wote wanamuhitaji Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Allaah hakihitaji chochote. Kusema kuwa yuko juu ya ´Arshi, au kusema kuwa amelingana juu ya ´Arshi, haina maana kuwa anaihitaji. Bali ´Arshi ndio inamuhitaji Allaah. Kwa sababu imeumbwa. Allaah ndiye anayezuia ´Arshi, mbingu na ardhi.

[1] 6:18

[2] 35:41

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 108-109
  • Imechapishwa: 18/08/2024