106. Ni ipi hukumu ya mapote haya kama al-Ikhwaan al-Muslimuun na Jamaa´at-ut-Tabliygh?

Swali 106: Ni ipi hukumu ya mapote haya kama al-Ikhwaan al-Muslimuun na Jamaa´at-ut-Tabliygh?

Jibu: Nchi yetu tuna kundi moja tu. Watu wake wote wa mijini na mashambani wanafata Qur-aan na Sunnah. Wanajenga urafiki na kupendana wao kwa wao.

Kuhusu makundi haya yaliyotujia, ni wajibu kuyakataa. Wanachotaka tupinde na kutugawanyisha na kumfanya mmoja awe Tabliyghiy, mwingine Ikhwaaniy na kadhalika. Ni kwa nini mgawanyiko huu? Kwa nini mgawanyiko huu? Huku ni kuikufuru neema ya Allaah kwa vile amesema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا

”Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane na kumbukeni neema ya Allaah juu yenu, pale mlipokuwa maadui, kisha akaunganisha nyoyo zenu, mkawa kwa neema Yake ndugu.”[1]

Sisi ni kundi moja, tuko na umoja na hali yetu iko wazi. Ni kwa nini tubadilishe kwa kitu kingine ambacho kiko chini kiubora? Ni kwa nini tuache kile ambacho Allaah (´Azza wa Jall) ametutunuku katika umoja, muungano na njia sahihi na tukaenda katika mapote yanayotutenganisha na kutugawanyisha na kufanya tukawa na chuki kati yetu. Mambo haya hayajuzu kabisa.

Mimi nimeona mwenyewe jinsi Jamaa´at-ut-Tabliygh wanavyoipuuza na kukimbia mbali na Tawhiyd. Nilikuwa kwenye msikiti mmoja Riyaadh na nilikuwa na muhadhara kuhusu Tawhiyd. Ndani ya msikiti kulikuweko kundi la Jamaa´at-ut-Tabliygh wamekusanyika. Nilipoanza kuzungumza tu wakatoka nje ya msikiti. Vivyo hivyo wamefanya katika nchi zingine na katika msikiti huohuo; wakatoka nje. Wanaposikia kunalinganiwa katika Tawhiyd wanatoka msikitini – ilihali wao ndio wanaita watu kukusanyika misikitini! Wala hawawakubalii watu wanaowalingania katika Tawhiyd. Hili haliwahusu wao tu bali ni kila ambaye anafuata mifumo iliyopangwa; hawakubali kupakana mafuta kwacho. Iwapo wameingia katika kitu hicho kwa ujinga basi pengine wakarejea katika haki. Lakini wameingia ndani ya jambo hili kwa sababu ya kufuata mfumo uliyopangwa tangu hapo zamani. Kwa ajili hiyo hawawezi kuacha mfumo wao. Wakifanya hivo ina maana wanayaacha mapote yao, kitu ambacho hawakitaki.

Kitabu cha mwisho kuhusu wao kimeandikwa na Shaykh Hamuud bin ´Abdillaah at-Tuwayjiriy (Rahimahu Allaah). Humo mmekusanywa maneno yao na ukosoaji wa watu wao ambao hapo kabla walikuwa nao kisha wakaachana nao. Ni kitabu kimekusanya na hakikuacha kitu kuhusu maudhui haya. Kwa sababu ni kitabu kipya na kimekusanya kila kilichosemwa juu yao na hivyo hakuna shaka yoyote iliyobaki.

Fitina huyapofosha macho. Vinginevyo ni vipi mtu ambaye amekulia juu ya Tawhiyd, ameisoma Tawhiyd na akaielewa Tawhiyd atadanganywa na watu hawa? Ni vipi atatoka pamoja nao[2]? Ni vipi atalingania kwao? Ni vipi atawatetea? Haya si kingine isipokuwa ni upotevu baada ya uongofu na kubadilisha kilicho kibaya kwa kilicho bora. Nawashauri watu wa kawaida wasitangamane nao.

[1] 3:103

[2] ´Allaamah ´Abdur-Razzaaq bin ´Afiyfiy amesema:

”Hawalingii katika Qur-aan na Sunnah. Wanalingania kwa Shaykh wao Ilyaas.” (al-Fataawaa (1/174))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 248-250
  • Imechapishwa: 18/08/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy