67. Washirikina wa sasa wanaabudu asiyekuwa Allaah katika hali zote

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Yule atayefahamu masuala haya ambayo Allaah kayaweka wazi katika Kitabu Chake – nayo ni kwamba washirikina ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita walikuwa wakimuomba Allaah (Ta´ala) na wakiomba asiyekuwa Yeye [wengine] katika kipindi cha raha, lakini katika kipindi kigumu na cha shida hawamuombi mwengine isipokuwa Allaah pekee asiyekuwa na mshirika na wanawasahau mabwana zao – itambainikia tofauti baina ya watu wa zama zetu na shirki ya watu wa mwanzo. Lakini ni nani ambaye moyo wake unayafahamu mambo haya ufahamu wa kina kabisa? Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada.

MAELEZO

Anabainisha (Rahimahu Allaah) kuwa washirikina wa zama zake walikuwa ni wabaya zaidi kuliko mshirikina wa zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mshirikina wa zama zake alikuwa akishirikisha wakati wa raha na wakati wa shida. Haya hayakuwa yakifanywa na washirikina wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walikuwa wakimuomba Allaah na wengine wakati wa raha tofauti na wakati wa shida hawamuombi mwengine isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall) peke Yake. Hii ni dalili yenye kuthibitisha kuwa shirki wakati wake (Rahimahu Allah) ilikuwa mbaya zaidi kuliko iliokuwa wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… imembainikia tofauti baina… “

Ataona tofauti kati ya mshirikina wa zama zake (Rahimahu Allaah) na mshirikina wa zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kadhalika ataona kuwa shirki ya watu wa zama zake ilikuwa mbaya zaidi kuliko shirki ya watu wa kale. Lakini ni kina nani ambao mioyo yao inayafahamu haya? Watu wengi hawayajui haya. Watu wengi yanawatatiza mambo na wanadhani kwamba batili ni haki na kinyume chake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 78
  • Imechapishwa: 25/11/2023