66. Radd kwa njia saba juu ya shubuha nne kubwa zilizotangulia

Halafu Shaykh akaraddi utata huu kwa njia saba muhimu:

Njia ya kwanza: Kufuru ya anayeamini baadhi ya hukumu za Kishari´ah na akazikufuru zingine.

Mwenye kuamini baadhi ya hukumu za Kishari´ah na akapinga zingine ni kama ambaye amekufuru zote. Watu hawa wamepinga Tawhiyd ambayo ndio waliokuja nayo Mitume. Nayo ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Watu hawa hawakumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Bali wamemshirikisha Yeye na wengine katika mawalii na waja wema. Uislamu haukubaliani na kuchukua sehemu na kuacha nyingine au kutenganisha. Uislamu mkubwa kabisa ni Tawhiyd na ndio ulinganizi wa Mitume wote. Watu hawa wamepinga jambo kubwa kabisa, ambalo ni kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah. Wamesema kuwa ni sawa mtu akamuwekea nadhiri na kumchinjia fulani kwa kuwa ni walii na kwamba walii ananufaisha na anadhuru, kama yalivyokuwa matendo ya washirikina wa mwanzo.

Njia ya pili: Shaykh (Rahimahu Allaah) ametaja uhalisia katika historia ya Kiislamu unaothibitisha ya kwamba wanachuoni katika kila zama wanamkufurisha yule mwenye kuamini baadhi ya vitu na akakufuru vyengine. Kwa mfano Maswahabah na waliokuja baada yao waliwapiga vita wale waliojidhihirisha kutamka shahaadah, kuswali, kufunga na kuhiji. Lakini pale walipofanya kitu katika shirki au wakapinga kitu katika dini wakawapiga vita na wakahalalisha damu na mali zao. Hayo ni kama ifuatavyo:

1- Banuu Haniyfah walioamini kuwa Musaylamah ni Mtume wa Allaah na pia wale waliokanusha uwajibu wa kutoa zakaah.

2- Katika wakati wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) aliwakufurisha wapetukaji waliokuwa wakisema kuwa ´Aliy ndiye Allaah pamoja na kuwa walikuwa wakishuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, wakiswali na wakifunga. Watu hawa walikuwa ni katika jeshi la ´Aliy. Lakini hata hivyo walipodhihirisha kupetuka mipaka ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) akawaunguza moto pamoja na kuwa wanashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Aliwaunguza pindi walipoamini kuwa kuna kiumbe ana haki ya kuabudiwa na hivyo akawakafirisha na akawaunguza na moto.

3- Wakati wa ´Abbaasiyyuun kulidhihiri pote “´Abbaasiyyuun` ambalo ni kundi moja wapo la Shiy´ah Ismaa´iyliyyah kwa kuwa wanajinasibisha na Ismaa´iyl bin Muhammad bin Ja´far. Ndio maana wakawa wameitwa Ismaa´iyliyyah. Vilevile wameitwa Faatwimiyyah kwa kuwa wanadai kuwa ni katika kizazi cha Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Ndio maana wakaitwa Faatwimiyyuun. Uhakika wa mambo wao ni katika mayahudi. Walidhihirisha Uislamu. Lakini kulidhihiri kutoka kwao mambo ya kikafiri na hatimaye mtawala wao akadai kuwa ni mungu kama alivyodai mtawala wa ´Ubaydiyyuun.

Maswahabah waliwapiga vita Banuu Haniyfah ilihali wanashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, wanafunga na wanahiji. Lakini walipoitakidi kuwa Musaylamah ni Mtume wakakufuru. Kwa kuwa yule mwenye kuitakidi kwa mtu baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba ni Mtume amekufuru ingawa atakuwa anaswali na kufunga. Kwa ajili hiyo ndio maana waislamu hii leo wamewakufurisha Qaadiyaaniyyah wanaosema kuwa Ahmad Qaadiyaaniy ni Mtume. Ikiwa yule anayemnyanyua mtu mpaka katika ngazi ya Mtume anakufuru, ni vipi asikufuru yule anayemnyanyua mtu katika ngazi ya Mola wa walimwengu na aidha akamtekelezea aina mbalimbali za ´ibaadah kama kumchinjia, kumuwekea nadhiri, kumuomba, kumtaka uokozi na mengineyo? Mambo ni kama alivyosema Shaykh kama walivyofanya baadhi ya watu kumnyanyua Taaj, Shamsaan na Yuusuf katika wakati wake na watu wakawapindukia kwa hoja ya kwamba eti ni mawalii na kwamba wana karama na mambo yasiyokuwa ya kawaida ilihali uhalisia wa mambo walikuwa wanafuata mfumo wa al-Hallaaj na Ibn ´Arabiy.

Njia ya tatu: Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wameweka mlango katika vitabu vya Fiqh na wakauita “Mlango kuhusu kuritadi” na wakataja ndani yake mambo yanayotengua Uislamu na wakataja mambo ambayo yanaweza kuwa madogo kwenye macho ya watu, lakini hata hivyo wakahukumu ya kwamba yule mwenye kuyafanya au kuyaitakidi amekufuru pamoja na kuwa anaswali, anafunga na anamuabudu Allaah. Mambo yanayomritadisha mtu hayakukomeka katika yale waliyoyataja.

Njia ya nne: Allaah amewahukumu kufuru watu waliotamka neno lililobatilisha Uislamu na imani yao. Amesema (Ta´ala):

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ

”Wanaapa kwa jina la Allaah kwamba hawakusema [maneno maovu]; ilihali wamesema neno la kufuru na wakakufuru baada ya Uislamu wao.” (09:74)

Wamekufuru kwa neno pamoja na kuwa walikuwa bega kwa bega pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakiswali na wakipambana Jihaad.

Njia ya tano: Allaah amewakafirisha watu kwa sababu ya neno walilotamka kwa njia ya mzaha na mchezo. Kukateremshwa juu yao:

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Ukiwauliza watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (09:65-66)

haya pamoja na kuwa wanaswali na walipigana vita bega kwa bega wakiwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk. Lakini hata hivyo walipotamka neno hili wakakufuru baada ya kuamini kwao na hayakuwafaa kitu kwa sababu wanaswali, wanafunga na wanapigana Jihaad.

Njia hizi zinabatilisha shubuha hizi. Uhakika wa mambo ni kuwa ni miongoni mwa utata mkubwa. Lakini hata hivyo majibu yake yako wazi na himdi zote anastahiki Allaah.

Njia ya sita: Shirki ya watu wa mwanzo inajumuisha kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutomsadikisha. Washirikina waliokuja nyuma wanasema kwamba wale ambao Qur-aan iliteremka juu yao hawashuhudii ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, wanamkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanapinga kufufuliwa, wanaikadhibisha Qur-aan na kuifanya kuwa ni uchawi ilihali wao wanashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhamamd ni Mtume wa Allaah, wanaisadikisha Qur-aan, wanaamini kufufuliwa, wanaswali na wanafunga. Vipi mtatufanya sisi kuwa ni kama wao? Anajibiwa kwa kuambiwa kuwa mtu akimsadikisha Allaah katika kitu na akamkadhibisha katika kitu kingine ni kafiri aliyeritadi kutoka katika Uislamu. Ni kama mfano wa wale wenye kuamini sehemu ya Qur-aan na wakapinga sehemu nyingine, kama wale wenye kukubali Tawhiyd, swalah na akapinga uwajibu wa zakaah, akakubali yote haya na akapinga uwajibu wa swawm, akayakubali yote haya na akapinga uwajibu wa hajj. Haijalishi kitu hata kama atakuwa anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.

Njia ya saba: Kufuru ya anayepinga uwajibu wa hajj hata kama atatamka shahaadah; ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, anaswali na anafunga. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ

“Hakika nyumba ya kwanza iliyowekwa kwa ajili ya watu ni ile iliyoko Bakkah yenye barakah na mwongozo kwa walimwengu.” (03:96)

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

“Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo wa kuiendea. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu.” (03:97)

Aayah inathibitisha kuwa anayepinga uwajibu wa hajj anakufuru hata kama atakuwa anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Ni vipi kuhusu yule anayekanusha Tawhiyd na akajuzisha kuyaabudu makaburi? Miongoni mwa dalili juu ya hayo ni yale Allaah aliyoeleza kuhusu Banuu Israa´iyl, pamoja na elimu na wema wao, walisema kumwambia Muusa:

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

”Tufanyie nasi mungu kama walivokuwa hawa wana mungu!” (07:138)

Vilevile baadhi ya Maswahabah walisema:

“Tufanyie Dhaat Anwaatw.”[1]

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaapa ya kwamba maneno haya ni kama mfano wa maneno ya Banuu Israa´iyl walipomwambia Muusa:

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

”Tufanyie nasi mungu kama walivokuwa hawa wana mungu!” (07:138)

[1] at-Tirmidhiy (2180) na Ahmad (05/218).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 100-103
  • Imechapishwa: 08/02/2017