67- Asipohudhuria mtawala wala naibu wake, basi atashika nafasi ya uimamu yule ambaye ni mjuzi zaidi wa Kitabu cha Allaah kisha kufuatia ule utaratibu ambao umepokelewa katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Awaongozeni watu yule ambaye ni msomi zaidi wa Kitabu cha Allaah. Wakiwa wanalingana katika kisomo basi mjuzi zaidi katika wao wa Sunnah. Wakiwa wanalingana katika Sunnah basi aliyetangulia kuhajiri. Wakiwa wanalingana katika kuhajiri basi aliyetangulia katika Uislamu. Wala mtu asimwongoze mwengine katika utawala wake na wala asiketi katika nyumba yake juu ya takrima yake isipokuwa kwa idhini yake.”
Ameipokea Muslim (03/133) na wengineo katika watunzi wa “as-Sunan” na “al-Masaanid” kupitia kwa Ibn Mas´uud al-Badr al-Answaariy. Nimeitoa katika “Swahiyh Abiy Daawuud” (nambari. 594, 598).
Awaswalishe yule ambaye ni msomi zaidi ijapokuwa ni kijana mdogo ambaye hajabaleghe. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Amr bin Salamah:
“Wao (yaani watu wake) walikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walipotaka kurudi wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nani atakayetuongoza kama imamu?” Akasema: “Ni yule katika nyinyi aliyekusanya zaidi Qur-aan” au “ambaye amechukua sehemu kubwa ya Qur-aan.” Hapakuwepo yeyote katika watu wangu ambaye amekusanya nilivokusanya mimi. Hivyo wakanitanguliza mbele kuswalisha na kipindi hicho mimi nilikuwa bado kijana mdogo ilihali nimevaa Shamlah. Hivyo sijawahi kuhudhuria mkusanyiko wowote wa kabila la Jarm isipokuwa mimi nilikuwa imamu wao. Na mimi ndiye nilikuwa nikiswalia majeneza yao mpaka hii leo.”
Ameipokea Abu Daawuud na al-Bayhaqiy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Msingi wake ni katika “al-Bukhaariy” na ndani yake hamna maeneo ya ushahidi. Na ni moja ya mapokezi ya Abu Daawuud. Nimeitoa katika “Swahiyh Abiy Daawuud” (nambari. 599, 500, 602).
68- Yakikusanyika majeneza mengi katika wanamume na wanawake, basi wataswaliwa swalah moja na watoto wa kiume – ijapo ni watoto wadogo – usawa wa imamu na majeneza ya wanawake yatawekwa usawa wa Qiblah. Kumepokelewa Hadiyth kadhaa juu ya hilo:
Ya kwanza: Naafiy´ amepokea, kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye amesema:
“Aliyaswalia[1] majeneza tisa yote kwa pamoja. Akayajaalia yale ya wanamme yako katika sawa wa kumkurubia imamu, yale ya wanawake yakawa usawa na Qiblah – akayapanga safu moja. Jeneza la Umm Kulthum, ambaye alikuwa msichana wa ´Aliy na ambaye ni mke ´Umar bin al-Khattwaab, likawekwa na la mtoto wake aliyekuwa akiitwa Zayd yakawekwa yote kwa pamoja na imamu kipindi hicho alikuwa ni Sa´iyd bin al-´Aasw. Miongoni mwa waliokuweko ni pamoja na Ibn ´Abbaas, Abu Hurayrah, Abu Sa´iyd na Abu Qataadah. Mtoto yule akamweka jirani na imamu. Bwana mmoja akasema: “Nikalipinga jambo hilo.” Nikamtazama Ibn ´Abbaas, Abu Hurayrah, Ibn Sa´iyd na Abu Qataadah na kusema: “Mambo gani haya?” Wakasema: “Ndio Sunnah.”
Ameipokea ´Abdur-Razzaaq (03/465, 2337), an-Nasaa´iy (01/280), Ibn-ul-Jaaruud katika “al-Muntaqaa” (267, 268), ad-Daaraqutwniy (194) na al-Bayahqiy (04/33).
Cheni ya wapokezi ya an-Nasaa´iy na Ibn-ul-Jaaruud ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim. al-Haafidhw katika “at-Talkhiysw” (05/276) amefanya mapungufu kuiegemeza kwa Ibn-ul-Jaaruud peke yake na akasema:
“Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”
Ama an-Nawawiy yeye amesema (05/224):
“Ameipokea al-Bayhaqiy kwa cheni ya wapokezi nzuri.”
Ya pili: ´Ammar, ambaye ni mtumwa aliyeachwa huru na al-Haarith bin Nawfal, ameeleza:
“Kwamba alishuhudia jeneza la Umm Kulthum na mtoto wake ambapo akamjaalia yule mtoto usawa wa imamu [mwanamke yule akawekwa nyuma yake na akamswalia.] Nikayapinga hayo. Katika watu waliokuweko hapo ni Ibn ´Abbaas, Abu Sa´iyd al-Khudriy, Abu Qataadah na Abu Hurayrah. [Nikawauliza juu ya hayo] ambapo wakasema: “Hii ni Sunnah.”
Ameipokea Abu Daawuud (02/66) na mtiririko ni wake, al-Bayhaqiy amepokea kutoka katika njia yake na an-Nasaa´iy. Ziada ni yake yeye. Cheni ya wapokezi ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim. an-Nawawiy (05/224) amesema:
“Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. ´Ammaar huyu alikuwa ni Taabiy´. Alikuwa ni mtumwa aliyeachwa huru na Banuu Haashim. Wamekubaliana juu ya uaminifu wake.”
al-Bayhaqiy amesema:
“Hammaad bin Salamah ameipokea mfano wake, kutoka kwa ´Ammar bin Abiy ´Ammaar pasi na kutaja namna ya uwekaji. Pia ametaja kwamba imamu alikuwa ni Ibn ´Umar. Miongoni mwa watu wao alikuweko al-Hasan, al-Husayn na Abu Hurayrah na karibu Maswahabah thamanini wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Pia ash-Sha´biy ameipokea ambaye yeye ametaja namna ya uwekaji kwa mfano wake. Ametaja kwamba imamu alikuwa ni Ibn ´Umar na hakutaja namna bwana yule alivyouliza swali. Amesema: “Nyuma yake alikuwa Ibn-ul-Hanafiyyah, al-Husayn na Ibn ´Abbaas. Katika upokezi mwingine imekuja: “´Abdullaah bin Ja´far.”
[1] Kwa msemo mwingine imamu kama unavyofahamisha mtiririko. al-Bayhaqiy ameyasema hayo wazi katika moja ya upokezi wake katika Hadiyth inayokuja baada yake kama tutakavyotaja hapa. Haya hayapingani na maneno yake baada ya hapo:
“… imamu kipindi hicho alikuwa ni Sa´iyd bin al-´Aasw.”
Kwa sababu makusudio ni kwamba yeye ndiye alikuwa mtawala. al-Haafidhw amesema:
“Kuna uwezekano kwamba Ibn ´Umar aliwaswalisha kikweli kwa idhini ya Sa´iyd bin al-´Aasw. Maneno yake:
“ … imamu kipindi hicho alikuwa ni Sa´iyd bin al-´Aasw.”
yanaweza vilevile kufasiriwa kwamba ndiye ambaye alikuwa mtawala kwa ajili ya kuoanisha kati ya mapokezi mawili.”
- Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
- Mfasiri: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 131-133
- Imechapishwa: 17/08/2020
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)