Kuhusu dalili zao kutoka katika Sunnah, zimepokelewa kwa mapokezi tele, kama alivosema ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika Haadiyl-Arwaah ilaa Bilaad-il-Afraah. Miongoni mwazo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi mwandamo usiku wa mwezi mwandamo – hamtosongamana katika kumuona Kwake.”[1]

Hamtohitajia kusongamana katika kumuona Allaah (´Azza wa Jall). Kila mmoja atamuona Mola akiwa mahali pake pasi na msongamano na mtu mwingine. Ni kama ambavyo watu wanaliona jua na mwezi pasi na kusongamana. Kikawaida ulimwenguni watu husongamana wanapoangalia kitu kilichojificha. Lakini kitu kikibwa kimenyanyuliwa juu, kama vile jua na  mwezi, basi kinaangaliwa pasi na msongamano; kila mmoja anakiona akiwa maeneo pake. Ikiwa mambo ni hivyo kwa viumbe viwili ambavyo ni jua na mwezi, tusemeje kuhusu Muumba (Subhaanahu wa Ta´ala)?

[1] al-Bukhaariy (554) na Muslim (633).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 75-76
  • Imechapishwa: 16/01/2023