64. Kuwa na subira katika kipindi cha raha

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Kila kinachomfika mja katika dunia hii ima iwe anakiridhia au hakiridhii. Ni lazima awe na subira katika hali zote mbili.

Kuhusu yale anayoyaridhia ni kama afya njema, usalama, nafasi, mali na starehe nyinginezo zinazoruhusiwa, anahitajia subira yenye upeo wa juu kabisa kutokana na sababu ya mambo yafuatayo:

1- Kwa sababu asiegemeze kwa hayo yaliyotajwa na akaghurika nayo. Hayo yaliyotajwa yasimfanye akawa na jeuri, mbaya au akawa na furaha yenye kulaumiwa isiyopendwa na Allaah.

2- Kwa sababu visimfanye akawa na tamaa na vikapata hukumu ya kinyume. Mwenye kula, kunywa na kufanya jimaa kwa kupindukia anapata hukumu ya kinyume na kula, kunywa na kujimai kunaharamishwa kwake.

3- Kwa sababu ya kuyatekelezea haki ya Allaah na asiyapuuze akaja kupokonywa.

4- Kwa sababu asivitumie katika haramu. Asiiachie nafsi yake akaenda katika kile inachotaka asije akatumbukia katika ya haramu. Akijihadhari, basi itamtumbukiza katika yanayochukiza. Hakuna walio na subira katika kipindi cha raha isipokuwa wale wakweli kabisa. Baadhi ya Salaf wamesema:

“Muumini na kafiri wote wawili wanasubiri juu ya misiba. Hakuna anayesubiri juu ya afya njema isipokuwa yule ambaye ni mkweli.”

Kuhusu yale asiyoyaridhia, yanaweza kuhusiana na upande wa ´ibaadah. Mja anahitaji subira kwayo. Asli ni kuwa nafsi haipendi aina mbalimbali za ´ibaadah. Isipokuwa tu yule ambaye amewafikishwa na Allaah. Hilo litabaini katika swalah ambapo mwanaadamu ameumbwa mvivu na kuipa kipaumbele raha na starehe. Hali kadhalika zakaah mwanaadamu ameumbwa bakhili na uchoyo. Inapokuja katika swawm mwanaadamu anataka kula na kunywa. Hataki kushinda na njaa. Na kadhalika.

Kwa hiyo mja ni mwenye kuhitaji subira na Allaah ndiye anajua zaidi. Kutoka katika mtazamo huu ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulipewa majaribio kwa madhara tukasubiri na tukapewa majaribio kwa wepesi hatukusubiri.”

Ni vigumu kuwa na subira wakati wa kipindi chepesi kwa sababu kuna uwezekano ikampelekea katika yale nafsi inayotamani. Mwenye njaa ana wepesi zaidi wa kusubiri wakati wa kukosa chakula kuliko pale anapokipata. Kuna wepesi zaidi wa kusubiri wakati wa kutokuwepo wanawake kuliko wakati wanapokuwepo. Aliye na kiu kikali ana wepesi zaidi ya kuvumilia kuliko kunapokuwepo maji.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 143-145
  • Imechapishwa: 03/11/2016