Swali 63: Kumeenea fikira mpya ambayo ni kutomfanyia Tabdiy´ ambaye anadhihirisha Bid´ah mpaka kwanza asimamishiwe hoja. Pasi na kurejea kwa wanazuoni wanaacha kumfanyia Tabdiy´ mpaka kwanza akinaine na Bid´ah yake. Ni upi mfumo wa Salaf juu ya jambo hili muhimu?

Jibu: Bid´ah[1] ni yale yaliyozuliwa katika dini. Yanaweza kuhusiana na kuzidisha, kupunguza au kubadilisha pasi na dalili ndani ya Qur-aan na Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote atakayezusha katika amri yetu yale yasiyokuwemo, atarudishiwa mwenyewe.”[2]

”Na nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu na kila upotofu ni Motoni.”[3]

Amesema (Ta´ala):

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu na wala msifuate badala Yake walinzi wengine – ni machache mnayoyakumbuka.”[4]

Kwa hivyo Bid´ah ni kuzusha jambo ndani ya dini. Haitambulishwi kwa maoni wala fikira za watu hawa. Jambo linarejea katika Qur-aan na Sunnah. Sunnah haihusiani na yale yanayofahamika kwa watu. Wala Bid´ah haihusiani na yale wasiyoyajua. Wala Sunnah haihusiani na yale yanayoridhiwa na watu. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hakututetegemezea akili wala maoni ya watu. Bali amtutosheleza kwa Wahy uliyotemremshwa kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sunnah ni yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mambo ya dini, Bid´ah ni yale ambayo hayakuletwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maneno na vitendo ndani ya dini. Hakuna yeyote aliye na haki ya kukihukumu kitu kuwa ni Bid´ah au Sunnah mpaka akipime kwa Qur-aan na Sunnah.

Kuhusu ambaye atafanya jambo linalokwenda kinyume na Qur-aan naa Sunnah kwa ujinga na akadhani kuwa ni haki na asiwe na ambaye atambainishia, ni mwenye kupewa udhuru kwa ujinga. Lakini wakati huohuo anakuwa mzushi. Pia kitendo chake hichi kinazingatiwa kuwa ni Bid´ah.

Nawashauri vijana ambao wanafata mfumo huu na wanayahukumu mambo kutegemea matamanio yao wamche Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na wasizungumze kuhusu dini isipokuwa kwa elimu na utambuzi. Haijuzu kwa mjinga kuzungumzia halali na haramu, Sunnah na Bid´ah, upotofu na uongofu pasi na elimu. Jambo hilo linaenda sambamba na shirki. Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika si vyenginevyo Mola wangu ameharamisha machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [aina zote] na ukandamizaji bila ya haki na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa ambayo hakukiteremshia mamlaka na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[5]

Ameambatanisha kuzungumza juu ya Allaah pasi na elimu pamoja na shirki. Inafahahamisha ukhatari wake katika dini. Kumsemea uwongo Allaah si kama kumsemea uwongo mwingine. Kumsemea uwongo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si kama kumsemea uwongo mwingine. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yeyote atakayenisemea uwongo kwa makusudi, basi ajiandalie makazi yake Motoni.”[6]

[1] Maana ya uzushi kilugha ni kuvumbua pasi na kutangulia kitu mfano wake hapo kabla. Maana ya uzushi kidini ni njia katika dini iliyovumbuliwa inayofanana na Shari´ah. Kunakusudiwa katika kuifuata njia hiyo kumwabudu Allaah (Subhaanah) kwa wingi. Tazama ”al-I´tiswaam” (1/50).

[2] Muslim (867).

[3] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[4] 7:3

[5] 7:33

[6] al-Bukhaariy (110) na Muslim (3).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 169-170
  • Imechapishwa: 26/06/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy