Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

54 – Kuonekana ni haki kwa watu wataokuwa Peponi – pasi na kumzunguka wala kulifanyia namna.

MAELEZO

Bi maana waumini kumuona Mola wao (Subhaanahu wa Ta´ala) huko Aakhirah. Watamuona kwa macho yao kama wanavyouona mwezi usiku wa mwezi mwandamo na kama wanavyoliona jua wazi kabisa pasi na mawingu, kama alivyoeleza hayo mteuliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh zilizopokelewa kwa mapokezi mengi. Ndio maana mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuonekana ni haki kwa watu wataokuwa Peponi.”

Bi maana ni kitu kimethibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hakuna ambao wameonelea kinyume isipokuwa tu wazushi na watu wenye ´Aqiydah zilizopinda.

Waumini watamuona Mola wao. Allaah (Subhaanah) amesema:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.”[1]

Bi maana nyuso za waumini zitafanywa nzuri na kung´arishwa. Kwa mujibu wa Aayah watamuona kwa macho yao, kwa sababu kihusishi (إِلَى) hutumiwa kwa kuona kwa macho. Kwa hivyo neno (النظر) lina maana nyingi, pindi linatajwa pamoja na kuhusishi (إِلَى) maana yake ni kutazama kwa macho:


أَفَلَا يَنظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ

“Je, hawamtazami ngamia namna walivyoumbwa?”[2]

Kwa msemo mwingine ni kwamba, hawaoni kwa macho yao viumbe hivi vya ajabu vinavyofahamisha juu ya uwezo wa Allaah? Vilevile katika Aayah iliyotangulia kuona (النظر) kumeatajwa na kihusishi (إِلَى).

Wakati neno hilo linatajwa lenyewe bila kihusishi mbele, maana yake ni kusubiri:

يَوْمَ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ لِلَّذِينَ آمَنُوا انظُرُونَا نَقْتَبِسْ مِن نُّورِكُمْ

“Siku wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike watakapowaambia wale walioamini: Tungojeeni, tupate mwangaza kutokana na nuru yenu!”[3]

Wanataka waumini wawasubiri ili wapate mwangaza wa nuru yao kwa sababu kipindi hicho nuru yao itakuwa imezimwa. Kipindi watakuwa gizani watataka waumini wawasubiri ili wapate sehemu ya nuru yao. Mfano mwingine ni:

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ

“Je, wanangojea nini isipokuwa Allaah awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika?”[4]

Bi maana hakuna kingine wanachosubiri isipokuwa kuja kwa Mola siku ya Qiyaamah ili ahukumu kati ya waja Wake.

Wakati mwingine neno (النظر) hutajwa na kihusishi (في). Katika hali hiyo inakuwa na maana ya kutafakari na kuzingatia. Amesema (Ta´ala):

أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ

“Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na vitu alivyoviumba Allaah?”[5]

Kwa nini hawazingatii viumbe vya Allaah vilivyoko juu mbinguni na chini ardhini ili wapate kuona uwezo wa Allaah na kustahiki kwake kuabudiwa?

Kwa hivyo neno kuona (النظر) limetajwa na kihusishi (إِلَى) na hivyo inakuwa na maana ya kuangalia kwa macho.

[1] 75:22-23

[2] 88:17

[3] 57:13

[4] 2:210

[5] 7:185

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 72-73
  • Imechapishwa: 16/01/2023