Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Allaah amewatunuku elimu na hekima ambavyo kwavyo wamewashinda wafuasi wa Mitume wengine wote, sembuse nyumati nyengine zisizokuwa na kitabu. Wamezizunguka elimu ambazo wengine wangelistahi kukabilishwa na wao. Ni vipi basi vile vizazi bora watakuwa na upungufu katika elimu na hekima, na khaswa inapokuja katika utambuzi juu ya Allaah na hukumu zinazohusiana na Aayah na majina na sifa Zake? Wako wapi wadogo hawa ukilinganisha na wao?

MAELEZO

Elimu ni utambuzi wa Qur-aan na Sunnah. Hekima ni kwamba wanakiweka kila kitu mahali pake stahiki na kwa ustadi. Kwa maana nyingine ni kwamba wanatenda kwa elimu hii kwa hekima na kwa ustadi. Hii ndio sifa ya wale wanazuoni waliobobea katika elimu.

Ummah huu kwa wanazuoni wake ndio ummah bora. Wametofautika kati ya nyumati zingine kwa sifa hii tukufu; Qur-aan, Sunnah na wanazuoni wenye mwenendo wa kiungu ambao katika zile nyumati nyenginezo zilizotangulia hakuna mfano wao. Nyumati zisizokuwa na kitabu, kama vile waabudia mizimu na wakanamungu, hawana maana yoyote katika utu. Watu wa Kitabu wamevipotosha vitabu vyao. Elimu ya ummah huu ukilinganishwa na elimu ya nyumati nyenginezo na zilizotangulia, basi kutapatikana tofauti kubwa. Kwa sababu Qur-aan hii ndio kitabu tukufu, bora na kipana zaidi. Aidha ni yenye kubaki mpaka siku ya Qiyaamah. Vitabu vyengine vyote vimepotoshwa na kubadilishwa. Isipokuwa tu Qur-aan hii ambayo Allaah ameihifadhi kutokana na makosa na kukengeushwa:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi Tumeteremsha Ukumbusho huu na hakika Sisi bila shaka ndio Tutakaouhifadhi!”[1]

Allaah ameihifadhi. Haikugeuzwa wala kubadilishwa. Itaendelea kuwa hivo mpaka siku ya Qiyaamah. Bado iko vilevile mbichi kama ilivyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuna yeyote anayepata ujasiri wa kubadilisha kitu ndani yake – hata herufi moja tu. Himdi zote njema anastahiki Allaah kwa hilo. Huku ni katika Allaah kuihifadhi na miujiza. Hili linafahamisha ubora wa Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ubora wa ummah huu. Ni vipi basi wanazuoni wa Salaf – ambao walikuwa katika zile karne bora – elimu yao itakuwa pungufu kuliko wale waliokuja nyuma, kama wanavosema wapotofu hawa ambao wanawaponda Salaf?

[1] 15:9

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 100-101
  • Imechapishwa: 13/08/2024