62. Nguzo ya kumi na nne ya swalah ni kumswalia ni Tasliym

Nguzo ya kumi na nne ni Tasliym ambazo ndizo zinamfanya mtu kutoka ndani ya swalah. Hilo ni kutokana na Hadiyth iliyokwishatangulia:

“Uharamu [ufunguzi] wake ni Takbiyr na uhalali [ufungwaji] wake ni Tasliym.”

Ibn-ul-Qayyim ameitaja katika kitabu chake “I’laam-ul-Muwaqqi’iyn” (2/358) na akasema:

”Hadiyth za kutoka katika swalah kwa kutoa Tasliym mbili zimesimuliwa kutoka kwa Maswahabah kumi na watano wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), zikiwa kati ya Swahiyh na nzuri. Wako wanazuoni wengine ambao wameona kuwa inatosha kutoa salamu moja tu. Hata hivyo maoni ya kutoa Tasliym mbili ndiyo yenye dalili nyingi. Isitoshe ndani yake kuna kuchukua tahadhari na kutoka katika makinzano ya wanazuoni. Hizi ni nguzo kumi na nne ambapo nguzo tano katika hizo ni za kimaneno:

1 – Takbiyr ya kufungulia swalah.

2 – Kusoma al-Faatihah.

3 – Tashahhud ya mwisho.

4 – Kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

5 – Tasliym.

Nguzo zilizobaki ni za kimatendo.

Shaykh Mar’iy bin Yuusuf  ametaja katika “Daliyl-ut-Twaalib”, uk. 33, kwamba nguzo za swalah ni kumi na nne ambapo akazingatia Tashahhud ya mwisho na kumswalia Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ni nguzo moja. Aidha akahesabu ndani yake kuinuka wima baada ya Rukuu´. Kuzingatia kuwa hiyo ni nguzo kumepokelewa dalili katika Hadiyth ya yule bwana aliyeswali kimakosa. Imekuja ndani ya Hadiyth hiyo:

”… kisha inuka mpaka unyooke sawasawa.”

Mtunzi wa kitabu amezingatia kuinuka wema baada ya Rukuu´ pamoja na kuinuka kutoka kwenye Rukuu´ kuwa ni nguzo moja. Ni kana kwamba anasema:

”Arukuu´ kutoka hapo mpaka anyooke wima sawasawa.”

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 87-89
  • Imechapishwa: 05/07/2026