Sunnah ni kuchelewesha daku muda wa kuwa mtu hachelei kuchomoza kwa alfajiri. Kwa sababu ndio kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Qataadah amepokea, kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Zayd bin Thaabit walikula daku. Pindi walipomaliza daku yao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimama kwa ajili ya kutaka kuswali na akaswali. Tukamuuliza Anas: “Kulikuwa muda kiasi gani kati ya kumaliza daku lake na kuingia kwake kuswali?” Akasema: “Ni kiasi cha mtu kusoma Aayah khamsini.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Bilaal alikuwa akitoa adhaana usiku. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Kuleni na kunyweni mpaka aadhini Ibn Ummiy Maktuum. Kwani hakika yeye haadhini mpaka ichomoze alfajiri.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Kuchelewesha daku ni kumfanyia upole zaidi mfungaji na kusalimika zaidi kutolala akapitwa na Fajr.

Mfungaji ana haki ya kula na kunywa mpaka pale atapokuwa na yakini ya kuingia kwa alfajiri. Hilo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi.”[1]

Anahukumu kuiona alfajiri ima kwa kuona kwa macho yake kwa juu au kwa taarifa zenye uhakika kupitia adhaana au njia nyingine. Kunapochomoza alfajiri ajizuie papo hapo na anuie kwa moyo wake na wala asitamke kwa mdomo wake. Kwa sababu kutamka nia kwa mdomo ni Bid´ah.

[1] 02:187

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 76
  • Imechapishwa: 26/04/2021