7- Mwenye kufa katika mji ambao hakuna ambaye atamswalia swalah ya hadhiri. Mtu huyu ataswaliwa na jopo la waislamu swalah ya ghaibu. Hilo ni kutokana na kitendo chake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumswalia an-Najaashiy. Kisa hicho kimepokelewa na jopo katika Maswahabah ambao baadhi wamezidisha juu ya wengine. Nimezikusanya Hadiyth zao kuhusu hiyo swalah kisha nikazitaja kwa mtiririko mmoja kwa ajili ya kukurubisha faida. Mtiririko ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Abu Hurayrah:

“Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatangazia watu [akiwa al-Madiynah] kuhusu an-Najaashiy [Aswhamah] [mfalme wa Uhabeshi] katika ile siku aliyokufa [Akasema: “Hakika ndugu yenu amefariki [Katika upokezi mwingine imekuja: “Leo amefariki mja mwema wa Allaah] [katika ardhi isiyokuwa yenu] [Hivyo simameni na mumswalie] [ Wakasema: “Ni nani?” Akasema: “an-Najaashiy] [Akasema: “Muombeeni msamaha ndugu yenu]. Wakaondoka kwenda mahali pa kuswalia. [Katika upokezi mwingine imekuja: “al-Baqiy´] [Kisha akasogea mbele na wakapanga safu nyuma yake] [safu mbili] [Tukapanga safu nyuma yake kama anavyopangiwa safu maiti na tukamswalia kama anavyoswaliwa maiti] [kama kwamba jeneza limewekwa mbele yake] akapiga Takbiyr [juu yake] Takbiyr nne.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/90, 154, 155, 157), Muslim (03/54) na tamko ni lake. Pia ameipokea Abu Daawuud (02/68, 69), an-Nasaa´iy (01/265, 280), Ibn Maajah (01/467), al-Bayhaqiy (04/49), at-Twayaalisiy (2300), Ahmad (02/241, 280, 289, 348, 438, 439, 479, 529) kupitia njia mbalimbali kutoka kwa Abu Hurayrah.

Ziada ya kwanza ni ya Muslim na Ahmad, ya pili ni ya al-Bukhaariy na ya tatu ni ya Ibn Maajah. Ya saba ni ya al-Bukhaariy na Muslim, an-Nasaa´iy na Ahmad. Ziada ya kumi na nusu yake ya pili ni ya Ahmad ambayo imekuja kwake kwa ukamilifu kutoka kwa Abu Hurayrah, kama itavyokuja. Ziada ya mwisho ni ya Muslim.

at-Tirmidhiy (02/140) amepokea kutoka kwake ambaye ameisahihisha kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimswalia an-Najaashiy ambapo akapiga Takbiyr nne. Ni moja pia katika mapokezi ya at-Twayaalisiy (2296).

2- Kisha al-Bukhaariy (03/145, 146) akaitoa, Muslim, an-Nasaa´iy, al-Bayhaqiy na at-Twayaalisiy (1681), Ahmad (03/295, 319, 355, 361, 363, 369, 4000) kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh).

Ziada ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano ni ya al-Bukhaariy na Muslim na Ahmad ambaye anayo pia ya tano na ya sita. Muslim na an-Nasaa´iy anayo ziada ya tisa. an-Nasaa´iy anayo jumla ya mwanzo katika ziada ya kumi. Ziada ya kumi na moja ni ya Muslim na Ahmad.

3- Kisha Muslim akaitoa, an-Nasaa´iy na at-Tirmidhiy (02/149) ambaye ameisahihisha. Pia na Ibn Maajah, Ibn Hibbaan, al-Bayhaqiy na at-Twayaalisiy (749), Ahmad (04/431, 433, 439, 441, 442) kutoka kwa ´Imraan bin Huswayn. Kuhusu hayo kuna ziada ya nne kwao wote. Ziada ya kumi iko kwa at-Twayaalisiy, an-Nasaa´iy, at-Tirmidhiy na Ahmad na kwake ndiko ipo ambayo iko baada yake na vivyo hivyo kwa Ibn Hibbaan.

4- Kisha akaitoa Ibn Maajah na at-Twayaalisiy (1068), Ahmad (04/07) kupitia kwa Abu Hudhayfah bin Asiyd. Kwao ipo ziada ya nne na ya tano juu yake. Vilevile kwao ipo ziada ya sita isipokuwa tu at-Twayaalisiy.

5- Kisha akaipokea Ibn Maajah na Ahmad (04/64 – 05/376) kutoka kwa Mujammiy´ bin Haarithah al-Answaariy. al-Buuswayriy amesema katika “az-Zawaa-id”:

“Cheni ya wapokezi ni Swahiyh na wapokezi wake ni waaminifu.”

Juu yake ziada ya nne na kwa Ibn Maajah ipo ziada ya tisa.

6- Kisha akaipokea at-Tirmidhiy na Ibn Maajah kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr mfano wa Hadiyth ya Abu Hurayrah kwa mukhtasari kwa at-Tirmidhiy. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh pia.

7- Kisha akaitoa Ahmad (04/264-263) kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa tamko lisemalo:

“Hakika ndugu yenu an-Najaashiy amefariki. Muombeeni msamaha.”

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

Katika Hadiyth hizi ipo dalili kwa njia mbalimbali juu ya kwamba an-Najaashiy, ambaye jina lake ni Aswhamah, alikuwa ni muislamu. Hayo yanatiliwa nguvu na kwamba kumepokelewa maandiko ya waziwazi kuhusu kusadikisha kwake utume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituamrisha kuondoka kwenda katika nchi ya an-Najaashiy – akataja kisa na ndani yake imekuja – an-Najaashiy akasema:

“Nashuhudia kwamba yeye ni Mtume wa Allaah na kwamba yeye ndiye ambaye alitolewa  bishara njema na ´Iysaa bin Maryam. Lau si huu ufalme nilionao basi ningelimwendea ili nimbebee viatu vyake.”

Ameipokea Abu Daawuud na al-Bayhaqiy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Hayo yamesemwa na al-Bayhaqiy katika yale yaliyonakiliwa na al-´Iraaqiy katika “Takhriyj-ul-Ahyaa´” (02/200). Pia Hadiyth hiyo iko na nyingine inayoitolea ushahidi kupitia kwa Ibn Mas´uud. Ameitoa at-Twayaalisiy (346). Ina shawahidi nyenginezo katika Musnad Ahmad (05/290, 292).

Tambua kwamba haya ambayo tumetaja kuhusu swalah ya ghaibu ndilo lile ambalo Hadiyth haitobeba sura nyingine zaidi yake. Kwa hili wametutangulia katika kulichagulia hili sehemu ya wahakiki wa madhehebu. Chukua ufupizo wa maneno ya Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika mazingira haya. Amesema katika “Zaad-ul-Ma´aad” (01/205, 206):

“Haikuwa katika uongofu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Sunnah zake kumswalia kila maiti aliye ghaibu au mbali. Wako wafu wengi wa waislamu waliofariki wakiwa mbali na hakuwaswalia. Imesihi kutoka kwake kwamba alimswalia an-Najaashiy kama anavyomswalia maiti. Hivyo wakatofautiana kuhusu hilo juu ya njia tatu:

1- Kwamba hii ni Shari´ah na Sunnah kwa Ummah wake kumswalia kila aliyefariki mbali. Haya ni maoni ya ash-Shaafi´iy na Ahmad.

2- Abu Haniyfah na Maalik wakasema kuwa hichi ni kitendo maalum kwake na si kwa mwengine.

3- Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah akasema:

“Maoni ya sawa ni kwamba mtu ghaibu akifariki katika nchi ambayo hakuswaliwa, basi ataswaliwa swalah ya ghaibu kama ambavo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimswalia an-Najaashiy. Kwa sababu alikufa kati ya makafiri na hakuswaliwa. Angeswaliwa huko alipofariki basi asingemswalia swalah ya ghaibu. Kwa sababu faradhi inadondoka kwa kule waislamu kumswalia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara alimswalia ghaibu na mara nyingine aliacha kufanya hivo. Kitendo chake kulifanya jambo na kukiacha kwake ni Sunnah. Jambo hili lina mahala pake. Allaah ndiye mjuzi zaidi. Kuna maoni matatu katika madhehebu ya Ahmad. Yenye nguvu zaidi ni huu upambanuzi.”

Wameyachagua haya baadhi ya wanachuoni wahakiki katika Shaafi´iyyah. al-Khattwaabiy amesema katika “Ma´aalim-us-Sunan” yafuatayo:

“Nimesema: “an-Najaashiy ni mtu muislamu ambaye alimwamini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamsadikisha juu ya utume wake. Isipokuwa tu alikuwa akiificha imani yake. Muislamu anapofariki basi ni lazima kwa waislamu kumswalia. Isipokuwa tu yeye alikuwa kati ya watu makafiri na hakupatikana katika hadhara yake ambaye atamtekelezea haki yake ya kumswalia. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akalazimika kufanya hivo. Kwani yeye ndiye Mtume wake, msimamizi wake na ambaye ana haki zaidi kwake. Hii – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ndio sababu iliyomfanya kumswalia swalah ya ghaibu.

Kujengea juu ya haya anapofariki muislamu katika mji miongoni mwa miji na haki yake ikapotea ya kumswalia, basi hawatomswalia wale walioko katika miji mingine mbali na yeye. Ikitambulika kuwa hakuswaliwa kwa sababu ya kikwazo, kizuizi au udhuru mwingine, basi Sunnah ni kumswalia na hilo halitoachwa kwa sababu ya umbali wa masafa. Akiswaliwa watu wataelekea Qiblah na hawatoelekea katika mji alioko maiti akiwa upande usiokuwa wa Qiblah.

Wapo wanachuoni wenye kuona kuwa imechukizwa kumswalia maiti aliyeko mbali na wakadai kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pekee ndiye amehusika kwa kitendo hichi kwa kuwa yuko katika hukumu ya anayemuona an-Najaashiy. Hayo ni kutokana na yale yaliyopokelewa katika baadhi ya Hadiyth eti “kwamba alisawazishiwa milima ya ardhi kiasi cha kwamba akawa anaona mahala pake[1]. Tafsiri hii ni mbavo. Kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapofanya kitu katika matendo ya Shari´ah basi ni lazima kwetu kumfuata na kumwigiliza. Jambo la umaalum halitambuliki isipokuwa kwa dalili. Miongoni mwa mambo yanayolibainisha hilo ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatoa watu kwenda uwanja wa kuswalia ambapo akawapangisha safu na wakaswali pamoja naye. Hivyo ikajulisha kuwa tafsiri hii ni mbovu – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.”

ar-Ruwyaaniy – ambaye pia na yeye ni as-Shaafi´iy – ameonelea yale aliyoonelea al-Khattwaabiy. Hayo ndio madhehebu ya Abu Daawuud pia. Kwani katika “Sunan” yake ameipa Hadiyth kichwa cha khabari chenye kusema “Mlango unaozungumzia juu ya kumswalia muislamu aliyekufa katika nchi ya shirki.” Wanachuoni wahakiki waliokuja baadaye kama mfano wa ´Allaamah Shaykh Swaalih al-Maqbaliy ameyachagua hayo kama ilivyo katika “Nayl al-Awtwaar” (04/43). Amejengea hoja kwa ziada ambazo zimejitokeza katika baadhi ya njia za Hadiyth:

“Hakika ndugu yenu amefariki katika ardhi isiyokuwa yenu. Hivyo simameni na mumswalie.”

Cheni ya wapokezi wake ni kwa mujibu wa al-Bukhaariy na Muslim.

Miongoni mwa mambo yanayozidi kutilia nguvu kwamba haikusuniwa kumswalia kila ambaye amefariki mbali ni kwamba wakati walipofariki makhaliyfah waongofu na wengineo hakuna yeyote katika waislamu ambaye aliwaswalia swalah ya ghaibu. Endapo wangeyafanya basi kungelipokelewa mapokezi mengi juu yao.

Haya yanakabiliwa na yale yanayofanywa na waislamu wengi hii leo pindi wanapomswalia kila aliyefariki mbali na khaswa akiwa na utajo na nafasi, ijapo ni kwa upande wa siasa peke yake, na hata hatambuliki kuwa ni mwema au ameutumikia Uislamu. Ijapokuwa mtu huyo amefariki katika msikiti mtakatifu wa Makkah na akaswaliwa na maelfu ya watu katika msimu wa hajj swalah ya papo kwa hapo. Yakabili yale mazingira tuliyoyataja kwa swalah kama hizi basi utajua kwa yakini kabisa kwamba ni katika mambo ya Bid´ah ambayo hakuna mwanachuoni yeyote anayejua Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na madhehebu ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) ataingiwa na shaka.

[1] an-Nawawiy (05/253) amesema katika ”al-Majmuu´” kwamba khabari hizi ni katika mambo ya kubuniwa. Kisha akaitaja Hadiyth ya al-´Alaa´ bin Zaydal kwamba ardhi ilikunjuliwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka akaenda kumswalia Mu´aawiyah bin Mu´aawiyah Tabuuk. Akasema kuwa ni Hadiyth hiyo ni dhaifu na kwamba imedhoofishwa na wanachuoni mabingwa akiwemo al-Bukhaariy na al-Bayhaqiy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 115-120
  • Imechapishwa: 13/08/2020