Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

51 – Pindi Allaah alipomtishia Moto aliyesema:

إِنْ هَـٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ

“Hii si chochote isipokuwa ni maneno ya mtu.”[1]

ndipo tukajua na kuyakinisha ya kwamba Qur-aan ni maneno ya Muumba wa watu na hayafanani na maneno ya watu.

MAELEZO

Mwenye kusema ya kuwa Qur-aan sio maneno ya Allaah na kwamba ni maneno ya mtu au ya Malaika ni kama mfano wa Waliyd bin al-Mughiyrah. Kuna tofauti gani kati ya hao wawili zaidi tu ya kwamba mmoja anadai kuwa ni muislamu tofauti na Waliyd bin al-Mughiyrah? Madai ya kudai Uislamu hayatoshi. Akiikufuru Qur-aan basi madai ya Uislamu hayatomfaa kitu, kwa sababu jambo hilo ni kuritadi. Haya yanatubainishia kuwa ni lazima kutambua kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah kikweli.

Lau Qur-aan ingelikuwa ni katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi kusingelikuwa lawama yoyote kwa Waliyd bin al-Mughiyrah aliyesema kuwa Qur-aan ni maneno ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vinginevyo ni vipi basi Allaah amtishie matishio haya makali? Ni dalili inayoonyesha kuwa alisema maneno makubwa na ya kutisha kwa kitendo chake cha kuinasibisha Qur-aan kwa asiyekuwa Allaah. Kila mwenye kushikamana na madhehebu haya na msimamo huu, basi atakuwa kama mfano wa Waliyd bin al-Mughiyrah kuna khatari juu yake kudumishwa Motoni milele.

[1] 74:25

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 71
  • Imechapishwa: 12/01/2023