60. Sura ya tatu: Kutanguliza swadaqah, nadhiri na zawadi kwa wafu, makaburi na kuyaadhimisha

Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefunga kila njia inayopelekea katika shirki na akatahadharisha matahadharisho ya hali ya juu. Miongoni mwayo ni masuala ya makaburi. Ameweka vidhibiti vinavyotuzuia kuyaabudu na kuchupa mipaka kwa watu wake. Miongoni mwa hayo:

1- Ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameonya kuchupa mipaka kwa mawalii na waja wema. Hayo ni kwa sababu yanapelekea katika kuyaabudu. Amesema:

“Tahadharini na kuchupa mipaka. Hakika si vyenginevo kilichowafanya kuangamia waliokuwa kabla yenu ni kuchupa mipaka.”[1]

“Msinisifu kwa kupitiliza kama manaswara walivyomsifu kwa kupitiliza ´Iysaa, mwana wa Maryam. Hakika mimi si vyenginevyo ni mja. Hivyo basi, semeni “Mja na Mtume Wake.”[2]

2- Ameonya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kujenga juu ya makaburi. Abul-Hayyaaj al-Asadiy amesimulia: “´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) alisema kunambia:

“Hivi nisikutume juu ya kazi aliyonituma kwayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Usiache picha hata moja isipokuwa umeiharibu wala kaburi lililoinuka isipokuwa umelisawazisha.”[3]

 3- Amekataza kuyatia chokaa na kuyajengea. Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kulitia chokaa kaburi, kulikalia na kulijengea juu yake jengo.”[4]

4- Ametahadharisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuswali kwenye makaburi. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anataka kufa alikuwa akijifunika kitambara usoni mwake. Anapohisi joto hukifunua na anasema akiwa katika hali hiyo: “Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni sehemu ya kuswalia.” Mtume akitahadharisha yale waliyokuwa wakiyafanya. Lau sikuchelea hilo basi kaburi lake lingewachwa nje, isipokuwa yeye alikhofia lisije kufanywa kuwa ni mahali pa kuswalia.”[5]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”[6]

Kuyafanya makaburi kuwa misikiti ni kule kuswali hapo ijapokuwa watu hawatojenga msikiti juu yake. Kila mahali mtu atakusudia kuswali sehemu hiyo basi kumefanywa msikiti. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimefanyiwa ardhi yote kuwa msikiti na yenye kutwahirisha.”[7]

Kukijengwa juu yake msikiti basi jambo linakuwa na ukhatari zaidi.

Watu wengi wamekwenda kinyume na makatazo haya na wakafanya yale aliyotahadharisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Matokeo yake wakatumbukia kwa sababu hiyo ndani ya shirki kubwa. Wamejenga juu ya makaburi misikiti, makuba na maqamat. Isitoshe wakayafanya ni sehemu ya matembezi ambapo hapo kunafanywa aina zote za shirki kubwa kama mfano wa kuyachinjia, kuwaomba waliyomo ndani yake, kuwataka msaada, kuwatekelezea nadhiri wao na mengineyo. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Atakayekusanya kati ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu makaburi, aliyoamrisha, aliyokataza na yale waliyokuwemo Maswahabah zake na yale waliyomo watu wengi hii leo basi ataona kuwa kimoja wapo kinapingana na kingine kwa njia ya kwamba kamwe hayakutani. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuswali kuyaelekea makaburi ilihali watu hawa wanaswali kwenye makaburi. Amekataza kuyafanya ni mahali pa kuswalia ilihali watu hawa wamejenga misikiti juu yake na wanaiita kuwa ni ´mashaahid` wakiiga nyumba za Allaah. Amekataza kuweka mataa juu yake  na watu wanakaa hapo kwa muda mrefu na kuwasha mataa juu yake. Amekataza kuyatembelea mara kwa mara na watu hawa wanayatembelea mara kwa mara na ´ibaadah za hijah na wanayakusanyikia kama wanavyokusanyika kwa ajili ya sikukuu au zaidi yake. Ameamrisha kuyasawazisha, kama alivyopokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kutoka kwa Abul-Hayyaaj al-Asadiy ambaye amesimulia: Abul-Hayyaaj al-Asadiy amesimulia: “´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) alinambia:

“Hivi nisikutume juu ya kazi aliyonituma kwayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Usiache picha hata moja isipokuwa umeiharibu wala kaburi lililoinuka isipokuwa umelisawazisha.”[8]

Katika “as-Swahiyh” yake pia kupitia kwa Thumaamah bin Shufiyy aliyesimulia:

“Tulikuwa na Fadhwaalah bin ´Ubayd katika ardhi ya Roma Ruudis akafariki rafiki yetu mmoja ambapo Fadhwaalah akaamrisha kaburi lake lisawazishwe kisha akasema: “Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiamrisha kuyasawazisha.”[9]

Watu hawa wanapitiliza katika kwenda kinyume na Hadiyth hizi mbili ambapo wanayanyanyua juu ya ardhi kama nyumba na wanayajengea makuba.” Mpaka aliposema: “Tazama tofauti hizi mbili kati ya yale aliyosunisha na akayakusudia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kukataza yale yaliyotangulia kutajwa juu ya makaburi na yale waliyosunisha watu hawa na wakayakusudia? Hapana shaka kwamba katika hayo kuna maharibifu ambayo mtu hawezi kuyadhibiti.”

Kisha akaanza kuyataja maharibifu hayo mpaka alipofikia kusema:

“Miongoni mwayo ni kwamba yale aliyosunisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati mtu anayatembelea makaburi ni kuikumbuka Aakhirah, kuwatendea wema wale wenye kutembelewa kwa kuwaombea du´aa, kuwatakia rehema, kuwaombea maghfirah na msamaha. Hivyo yule mwenye kuyatembelea anakuwa ameifanyia wema nafsi yake mwenyewe na yule maiti.  Washirikina hawa wakayapindua mambo na wakaifanya dini kinyumenyume ambapo wakafanya malengo ya yale matembezi ni kumshirikisha maiti, kumuomba, kuomba kupitia kwake, kumuomba haja zao, kuteremsha baraka kutoka kwao, wawanusuru dhidi ya adui zao na mfano wa hayo. Wakawa ni wenye kuzifanyia vibaya nafsi zao wenyewe na yule maiti. Inatosha kumkosesha yule maiti baraka alizosunisha katika kumuombea du´aa, kumuombea rehema na msamaha.”[10]

Kwa haya inapata kubainika kutanguliza nadhiri na mambo ya kujikurubisha kwa wale watembelewaji ni shirki kubwa. Sababu yake ni kwenda kinyume na mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hali ambayo ni lazima kaburi liwe juu yake kwa kutolijengea jengo na misikiti juu yake. Kwa sababu ikijengewa makuba, misikiti pambizoni mwake na mahali pa kutembelewa wajinga watafikiria kuwa wale waliozikwa mahali hapo wananufaisha na wanadhuru, wanawasaidia wale wenye kuwataka msaada na wanatatua haja mbalimbali za wale wenye kuwaelekea. Matokeo yake watawatekelezea nadhiri na mambo ya kujikurubisha mpaka wawe kama masanamu yenye kuabudiwa badala ya Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Usilifanye kaburi langu kuwa ni sanamu lenye kuabudiwa.”[11]

Hakuomba du´aa hii isipokuwa ni kwa sababu kutatokea kitu katika hayo, jambo ambalo limetokea kwenye makaburi katika miji mingi ya Kiislamu. Kuhusu kaburi lake Allaah amelilinda kutokana na baraka za du´aa yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ingawa kunaweza kutokea ndani ya msikiti wake kitu katika wendaji kinyume kutoka kwa baadhi ya wajinga au makhurafi. Lakini hata hivyo hawawezi kulifikia kaburi lake. Kwani kaburi lake liko nyumbani kwake na sio msikitini na isitoshe limezungukwa na kuta. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema katika “an-Nuuniyyah” yake:

Akamuitikia Mola wa walimwengu

na akalizungusha kuta tatu

[1] Ahmad (3248) na Ibn Maajah (3029).

[2] al-Bukhaariy (3445).

[3] Muslim (2240).

[4] Muslim (2242).

[5] al-Bukhaariy (436) na Muslim (531).

[6] Muslim (532).

[7] al-Bukhaariy (438) na Muslim (1163).

[8] Muslim (969).

[9] Muslim (968).

[10] Ighaathat-ul-Lahfaan (01/215-217).

[11] Maalik (475).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 110-114
  • Imechapishwa: 24/03/2020